Vijiti au vipandikizi ni vipande vidogo vya plastiki vyenye umbo kama njiti za kiberiti ambavyo hutoa vichocheo vya progestin kwenye mwili wa mwanamke.
Ni mojawapo ya njia za kisasa za uzazi wa mpango.
Vichocheo hivi hufanana na vile ambavyo mwili wa mwanamke huvizalisha, kwa jina ni progesterone.
Mtaalamu wa afya aliyepata mafunzo maalum, kwa kutumia kifaa maalum huingiza kwenye sehemu ya juu ya mkono kijiti kimoja, au vijiti viwili chini ya ngozi ya eneo hilo.
Aina
Kuna aina nyingi za vipandikizi. Mojawapo ya aina hizo ni
- Jadelle, huwa na mjumuisho wa vijiti viwili na hufanya kazi kwa miaka 5.
- Implanon NXT (Nexplanon), huwa ni kijiti kimoja ambacho hufanya kazi kwa wastani wa miaka 3
- Levoplant (Sino-Implant II), huwa na mjumuisho wa vijiti viwili na hufanya kazi kwa miaka 4
- Norplant, ilijumuisha vidonge 6 na ilifanya kazi kwa miaka 5-7. Matumizi yake yaliondolewa mwaka 2018.
Hufanya Vipi Kazi?
Vijiti hutumia mifumo miwili katika kuzuia ujauzito.
Huzuia uzalishwaji wa yai lililo komaa pamoja na kutengeneza ute mzito kwenye mlango wa kizazi ambao huzuia mbegu za mwanamme zisifikie yai.
Ufanisi
Njia hii hufanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Ni wastani wa mwanamke mmoja tu katika kundi la wanawake 1000 ndiyo hupata ujauzito baada ya kutumia njia hii.
Mfano, kwa wanawake wanene sana ufanisi wa vipandikizi aina Jadelle na levoplant hupungua nguvu kadri muda wa mwisho wa matumizi unavyokaribia.
Watu hawa hushauriwa kubadili kipandikizi mapema kabisa ya tarehe muafaka za kufanya hivyo.
Faida
Ukiondoa faida ya kukinga ujauzito, aina hii ya uzazi wa mpango husaidia kumkinga mwanamke asipatwe na tatizo la upungufu wa damu, hupunguza uwezekano wa kupatwa na ujauzito ulio nje ya mji wake pamoja na kupunguza dalili za maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo wa uzazi.
Maudhi
Kama zilivyo njia zingine za uzazi wa mpango, vijiti hubeba pia maudhi kadhaa ambayo baadhi yake ni kukosekana kabisa kwa hedhi, kuvurugika kwa mpangilio wa hedhi, maumivu ya kichwa, maumivu ya sehemu ya chini ya tumbo, Chunusi, kuongezeka kwa uzito, kuwasha kwa matiti, kizunguzungu, hasira pamoja na kiungulia.
Nani Anaweza Kutumia?
Njia hii inaweza kutumiwa karibia na kila mwanamke. Inafaa kwa mwanamke aliyewahi kupata mtoto, mwanamke ambaye hajawahi kupata mtoto, mwanamke aliyeolewa na asiye olewa, mwenye umri wowote, hata walio na zaidi ya miaka 40, waliopitia kipindi cha kutoa ujauzito, kuharibika kwa ujauzito au waliopata ujauzito uliotungwa nje ya mji wake, wanawake wanaonyonyesha, wenye changamoto ya upungufu wa damu pamoja na wale wenye VVU wanaotumia dawa na wasio tumia dawa.
Nani Hapaswi Kutumia?
Mtoa huduma anapswa kufanya uchunguzi wa kina kubaini uwepo wa hali kadhaa za kiafya zinazoweza kutoa mapendekezo ya kutokutumika kwa njia hii.
Baadhi ya wanawake wenye hali hizi hawaruhusiwi kutumia njia hii;
Uwepo wa damu iliyoganda kwenye mishipa ya miguu au mapafu, kutokwa na damu za mara kwa mara wakati wa ovulation, kwenye saratani ya matiti, mwenye uvimbe kwenye ini, au uwepo wa tatizo lolote kubwa kwenye ini, mwenye tatizo la kinga mwili linaloitwa lupus erythematosus pamoja na yule mwenye ujauzito tayari.
Masharti ya Kuweka
Kama alikuwa anatumia kalenda
Kama mwanamke ataweka kijiti ndani ya siku 7 tangu aanze hedhi atakingwa kwa asilimia 100 dhidi ya ujauzito.
Ikiwa ataweka baada ya siku 7 za hedhi, itabidi atumie njia nyingine mbadala kujikinga na ujauzito ndani ya siku 7 za mwanzo za uwekwaji wa kijiti hiki.
Kama alikuwa anatumia majira
Huwekwa hapohapo baada ya kuacha kutumia majira.
Mwanamke hana haja ya kusubiri hadi hedhi ionekane.
Kama ananyonyesha kwa asilimia 100
Ikiwa hedhi haijarudi anaweza kuweka muda wowote ndani ya miezi 6 ya mwanzo.
Ikiwa ataweka muda ambao hedhi imerudi, anapaswa kufanya hivyo ndani ya siku 7 za hedhi ili apate kinga kamili.
Kama ataweka baada ya siku 7 za hedhi yake, anashauriwa kutumia njia mbadala kujikinga walau ndani ya siku 7 za mwanzo za uwekwaji wa kijiti hiki.
Wanao nyonyesha kidogo
Ikiwa hedhi haijarudi, anaweza kuweka muda wowote.
Ikiwa ataweka muda ambao hedhi imerudi, anapaswa kufanya hivyo ndani ya siku 7 za hedhi ili apate kinga kamili.
Kama ataweka baada ya siku 7 za hedhi yake, anashauriwa kutumia njia mbadala kujikinga walau ndani ya siku 7 za mwanzo za uwekwaji wa kijiti hiki.
Wasio nyonyesha kabisa
Ikiwa ataweka kijiti hiki ndani ya wiki 4 za mwanzo tangu ajifungue atakuwa salama kwa asilimia 100.
Kama ataweka kijiti baada ya wiki 4 za kwanza na ikiwa hedhi yake haijarudi, atapaswa kutumia njia mbadala ya kujikinga siku 7 za mwanzo za matumizi ya njia hii.
Kama ataweka kijiti baada ya wiki 4 za kwanza na ikiwa hedhi yake imerudi, atapaswa kufanya hivyo ndani ya siku 7 za mwanzo za hedhi ili apate kinga kamili.
Aidha, ikiwa ataweka baada ya siku 7 za hedhi ya mwezi husika apaswa kutumia njia mbadala ya uzazi wa mpango kujikinga ili asipate ujauzito ndani ya siku 7 za mwanzo za uwekwaji wa kijiti.
Mwanamke asiyepata kabisa hedhi
Anaweza kuweka kijiti hiki muda wowote. Siku 7 za mwanzo anashauriwa kutumia njia mbadala kujikinga na ujauzito.
Aliyetoa ujauzito au ujauzito umeharibika
Anaweza kuweka moja kwa moja baada ya tukio hili.
Ikiwa ataweka baada ya siku 7 tangu tukio husika litokee, atapaswa kutumia njia mbadala kujilinda siku 7 za mwanzo ili asipate ujauzito.
Muhimu
Vijiti hivi baada ya kutolewa nje ya mwili wa mwanamke huwa havina uwezo wa kuzuia ujauzito usitungwe. Vichocheo huwa havibaki ndani.
Ikitokea mwanamke kaacha kuona hedhi yake baada ya kutumia kijiti asiwe na wasiwasi. Hii haina tofauti na kuacha kuona hedhi wakati wa ujauzito.