Depo Provera: Njia ya Kisasa ya Uzazi wa Mpango

6 Min Read

Hizi ni sindano zilizo tengenezwa kwa kutumia vichocheo vya progestin. Vichocheo hivi hufanana na vile vinavyo patikana ndani ya mwili wa mwanamke.

Sindano hii huitwa Depot Medroxyprogesterone acatate (DMPA) au maarufu zaidi kama Depo provera.

Baada ya kuchomwa kwenye msuli wa mwili, au chini ya ngozi, sindano hii huanza kutoa vichocheo vyake polepole.

Majina mengine maarufu ya sidano hii ni Depo au petogen. Hufanya kazi kwa kuzuia mwili wa mwanamke usitoe mayai yaliyo pevuka

Ufanisi

Hutegemea na namna gani mwanamke anapata sindano hii kwa wakati.

Katika wanawake 100 wanaotumia aina hii ya sindano, wanawake 4 kati yao hupata ujauzito. Sababu kuwa ni kutokupata sindano hii kwa wakati sahihi.

Ikiwa kila mwanamke atapata sindano hii kwa wakati, nafasi ya kubeba ujauzito hupungua kabisa, karibia sifuri.

Muda wa Dozi

Sindano hii huchomwa kila baada ya miezi 3 au baada ya wiki 13. Mwanamke anaweza kupata sindano hii mapema zaidi kwa wiki 2 kabla ya muda sahihi.

Ikiwa zaidi ya wiki 4 zitapita pasipo kupata muendelezo wa dozi kutoka kwenye tarehe sahihi ya kupata dozi hii, mwanamke anashauriwa kujikinga kwa kutumia njia mbadala ili asipate ujauzito hadi pale atakapo choma sindano hii.

Maudhi

Sindano za Depo provera (DMPA) huwa na maudhi yafuatayo;

Kuvurugika kwa hedhi hasa miezi 3 ya mwanzo, kukosekana kabisa kwa hedhi, hasa mwaka wa kwanza wa matumizi, kuongezeka kwa uzito wa mwili, maumivu ya mara kwa mara ya kichwa, kizunguzungu, hasira, kupungua kwa hamu ya tendo la ndoa pamoja na kupungua kwa ujazo wa mifupa.

Faida Zake

    Ukiachia maudhi ya sindano hii, pamoja na sifa yake kuu ya kuzuia ujauzito, faida zingine pia huhusishwa moja kwa moja ni kuzuia saratani ya mji wa uzazi, kuzuia uvimbe kwenye mji wa uzazi, kufuta dalili za ugonjwa wa PID pamoja na kupunguza maumivu ya kiuno, nyonga na sehemu ya chini ya mgongo

    Nani anaweza kutumia?

    Karibia kila mwanamke asiye na ujauzito kwa wakati huo anaweza kutumia aina hii ya njia ya uzazi wa mpango. 

    Mwenye mtoto tayari, au ambaye hajawahi kupata mtoto, aliyeolewa na asiye olewa, mwanamke aliyeharibikiwa ujauzito, mwanamke anayevuta sigara, mwanamke anayenyonyesha, kuanzia wiki 6 baada ya kujifungua pamoja na wanawake wenye VVU.

    Tofauti na ilivyo kwa vidonge vya majira, sindano hii inaweza kutolewa pia kwa mwanamke mwenye shinikizo la juu la damu 

    Mwanamke mwenye historia ya kuugua saratani ya matiti, kiharusi, kisukari, magonjwa ya moyo, wenye ujauzito tayari pamoja na wale wanaotokwa na damu kabla ya ovulation hawashauriwi kutumia aina hii ya uzazi wa mpango.

    Masharti ya Kuchoma

    Kama anatumia kalenda

    Kama mwanamke atachoma sindano hii ndani ya siku 7 tangu aanze hedhi atakingwa kwa asilimia 100 dhidi ya ujauzito.

    Ikiwa atachoma baada ya siku 7 za hedhi, itabidi atumie njia nyingine mbadala kujikinga na ujauzito ndani ya siku 7 za mwanzo za uchomwaji wa sindano hii.

    Kama anatumia majira

    Huchomwa hapohapo baada ya kuacha kutumia majira. Mwanamke hana haja ya kusubiri hadi hedhi ionekane.

    Kama ananyonyesha kwa asilimia 100

    Anapaswa kusubiri hadi anyonyeshe walau kwa wiki 6.

    Ikiwa atachoma muda ambao hedhi imerudi, anapaswa kufanya hivyo ndani ya siku 7 za hedhi ili apate kinga kamili.

    Kama atachoma baada ya siku 7 za hedhi yake, anashauriwa kutumia njia mbadala kujikinga walau ndani ya siku 7 za mwanzo za uchomwaji wa sindano.

    Wanao nyonyesha kidogo

    Anapaswa kusubiri hadi anyonyeshe walau kwa wiki 6.

    Ikiwa atachoma muda ambao hedhi imerudi, anapaswa kufanya hivyo ndani ya siku 7 za hedhi ili apate kinga kamili.

    Kama atachoma baada ya siku 7 za hedhi yake, anashauriwa kutumia njia mbadala kujikinga walau ndani ya siku 7 za mwanzo za uchomwaji wa sindano.

    Wasio nyonyesha kabisa

    Anaweza kuchoma sindano hii muda wowote tu pasipo kusubiri.

    Ikiwa atachoma muda ambao hedhi imerudi, anapaswa kufanya hivyo ndani ya siku 7 za hedhi ili apate kinga kamili.

    Kama atachoma baada ya siku 7 za hedhi yake, anashauriwa kutumia njia mbadala kujikinga walau ndani ya siku 7 za mwanzo za uchomwaji wa sindano.

    Asiyepata kabisa hedhi

    Anaweza kuchoma sindano hii muda wowote.

    Siku 7 za mwanzo anashauriwa kutumia njia mbadala kujikinga na ujauzito.

    Aliyetoa ujauzito au ambaye ujauzito umeharibika

    Anaweza kuchoma moja kwa moja baada ya tukio hili.

    Ikiwa atachoma baada ya siku 7 tangu tukio husika litokee, atapaswa kutumia njia mbadala kujilinda siku 7 za mwanzo ili asipate ujauzito.

    Muhimu

    Kuongezeka uzito walau kwa kiasi cha 1 -2 kg kila mwaka wakati wa matumizi ya sindano hii ni jambo la kawaida.

    Wanawake wanaotumia Depo provera huchelewa kwa wastani wa miezi 4 hadi 10 kwenye kupata ujauzito kuliko wanawake wanaotumia njia zingine. Kiasi cha muda aliotumia sindano hii hauhusiki katika kuamua ni lini atapata tena ujauzito.

    Baadhi ya wanawake huenda mbali zaidi kwa huchelewa kwa zaidi ya miezi 12 katika kupata ujauzito.

    Muhtasari

    Mwanamke anaweza kuchelewa hadi wiki 4 kupata sindano hii kutoka tarehe ya mbele ya dozi inayofuata na bado asiwe na uwezo wa kupata ujauzito.

    Kwa mujibu wa taarifa rasmi za Taasisi ya American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG), sindano hizi hupunguza ujazo wa mifupa hivyo kuongeza nafasi ya mwanamke kupatwa na changamoto za mifupa ikiwemo pamoja na kuvunjia kirahisi kwa mifupa baada ya kufikia umri wa ukomo wa hedhi.

    Share This Article