Ni michubuko inayotokea kwenye kuta za mfumo wa chakula, hasa kwenye sehemu ya tumbo au pia sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo.
Ukubwa wa vidonda hivi hutofautiana, kuanzia millimita chache hadi sentimita kadhaa.
Hutenganishwa na michubuko ya kawaida kutokana na namna vinavyo chimba kuta za mfumo wa chakula.
Pia vinaweza kutokea kwenye umri wowote, kuanzia utotoni hadi uzeeni.
Vyanzo
Kuna nadharia nyingi zinazohusishwa na kutokea kwa vidonda vya tumbo. Lakini ukweli ni kuwa, kuna vyanzo vikuu viwili tu ambavyo ni maambukizi ya bakteria wabaya jamii ya H. pylori pamoja na dawa za kupunguza maumivu zinazopatikana kwenye kundi la NSAID’s mfano aspirin, ibuprofen na diclofenac
Tabia Hatarishi
Uvutaji wa sigara ni tabia hatarishi inayosaidia kutokea kwa tatizo hili pamoja na kuongeza ukubwa wa athari zake.
Hupoozesha pia kasi ya uponaji kwa wagonjwa, pamoja na kuongeza uwezekano wa kujirudia tena kwa ugonjwa baada ya kupona.
Pombe, stress pamoja na kuzaliwa kwenye familia yenye historia ya uwepo wa ugonjwa huu huongeza nafasi ya kupatwa na shida hii.
Dalili
Mara nyingi hutegemea umri pamoja na eneo husika vilipo vidonda hivi na baadhi ya dalili hizo ni Maumivu makali ya kuvuta kwa misuli, au kuwaka moto kwa misuli ya tumbo na kujaa gesi mara kwa mara, kiungulia, kichefuchefu, choo chenye damu, au choo cheusi, kutapika uchafu wenye damu, au wenye rangi ya weusi, kupata maumivu kifuani, kama moto unaochoma pamoja na kujihisi kushiba kirahisi, hata baada ya kukaa na njaa kwa muda mrefu
Kwa wale ambao vidonda hivi vipo kwenye sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo hupatwa na maumivu karibia kila muda.
Wakati wa asubuhi maumivu huwa makali zaidi na hutokea tena baada ya masaa mawili au matatu baada ya mlo. Maumivu haya huwapo pia wakati wa usiku, na mara nyingi huwaamsha kutoka usingizini.
Vipimo
Historia ya maisha yako itachukuliwa ili kufuatilia chanzo na athari za ugonjwa huu.
Ili kuthibitisha kuwa vidonda hivyo vinasababishwa na bakteria au la, choo, damu au hewa vitachukuliwa ili kufanyiwa uchunguzi.
Aina nyingine pia za vipimo zinaweza kufanyika kwa kadri ambavyo daktari ataona inafaa.
Tiba
Msingi wa matibabu ya vidonda vya tumbo hujumuisha mambo mawili ambayo ni uangamiza bakteria wa H. pylori pamoja na kutumia dawa za kudhibiti uzalishwaji wa asidi.
Udhibiti wa asidi na vimelea huhitajika sana. Matumizi ya dawa za antibayotiki hufaa wakati huu, pia dawa za kudhibiti uzalishwaji wa asidi nyingi hupaswa kumezwa.
Baadhi ya dawa zinazoweza kutumika ni Rabeprazole, Omeprazole, Pantoprazole, Ranitinide, Tinidazole nk.
Ikiwa changamoto hii itaendelea kujirudia, pia ikiwa changamoto zinazosababishwa na ugonjwa huu kama vile kuziba kwa utumbo au kuvuja kwa damu tumboni, upasuaji huwa ni chaguo sahihi.
Kinga
Ni muhimu sana kuepuka uvutaji wa sigara pamoja na kuepuka matumizi ya mara kwa mara ya dawa za kutuliza maumivu, hasa pasipo kufuata ushauri wa mfamasia au daktari.
Ili kujikinga na kurudia kwa mara kwa mara kwa tatizo hili, mgonjwa anashauriwa kumeza vizuri dawa zake hasa ikiwa tatizo hili limesabababishwa na vimelea vya H. pylori ili kuviangamiza kabisa.
Baadhi ya tafiti zimeelezea pia mchango wa vyakula katika kutibu tatizo la vidonda vya tumbo.
Asali, mboga za majani hasa spinachi, kabichi, broccoli, matunda kama apple, vitunguu saumu, binzari pamoja na mafuta ya mzeituni husaidia kutibu ugonjwa huu.
Muhtasari
Katika nyakati chache sana, ugonjwa huu unaweza kusababisha kuvujia kwa damu nyingi tumboni, saratani ya tumbo pamoja na kuziba kwa utumbo.
Ili kutokufikia hali hizi, ni muhimu kupata matibabu ya haraka na sahihi kuanzia pale unapohisi kuwa na tatizo hili.