Chanzo, Dalili, Athari na Tiba za Ugonjwa wa Kisukari (Diabetes)

5 Min Read

Kisukari ni ugonjwa sugu unaotokea baada ya tezi za kongosho kushindwa kuzalisha vichocheo vya kutosha vya insulin, au mwili ukipoteza sifa na uwezo wa kuvitumia vichocheo vya insulin vinavyozalishwa ndani yake.

Insulin ndio vichocheo vinavyotumiwa na mwili katika kudhibiti ongezeko la sukari.

Hivyo, kwa lugha rahisi kabisa, kisukari kama jina lake lilivyo ni ugonjwa unaotokea baada ya mwili kushindwa kudhibiti ongezeko la sukari kwenye kiwango cha kawaida kinachotakiwa.

Aina Zake

Kuna aina nyingi za kisukari, lakini wataalamu hupenda kuugawa ugonjwa huu kwenye aina kuu tatu ambazo ni kisukari aina ya kwanza, kisukari aina ya pili pamoja na kisukari cha ujauzito.

Aina ya kwanza ya kisukari hutokea baada ya mwili kukosa sifa na uwezo wa kuzalisha vichocheo vya insulin. Mara nyingi husababishwa na mwili wenyewe kuzishambulia seli zinazozalisha vichocheo hivi. Walau asilimia 10 ya wagonjwa wote wa kisukari huwa wapo kwenye kundi hili.

Aina ya pili ya kisukari hutokea kwa watu ambao miili yao huzalisha vichocheo vya insulin, lakini huwa sugu kiasi cha kushindwa kuvitumia kikamilifu katika kudhibiti sukari. Walau asilimia 90 ya wagonjwa wote wa kisukari huwa wapo kwenye kundi hili.

Kisukari cha ujauzito hutokea wakati wa ujauzito pekee. Husababishwa na baadhi ya vichocheo ambavyo mwili wa mwanamke huvitengeneza ili kumlinda mtoto. Wanawake wenye uzito mkubwa, pamoja na wale ambao wakati wa ujauzito huongezeka sana uzito huwa kwenye hatari kubwa ya kupatwa na aina hii ya kisukari.

    Visababishi

    Uchache wa vichocheo vya insulin au kupungua kwa msisimko wake kwenye kudhibiti ongezeko la sukari ndio kisababishi namba moja cha ugonjwa wa kisukari.

    Lakini baadhi ya tabia, mtindo wa maisha pamoja na mambo mengine yanayozunguka maisha ya mtu hutoa mchango mkubwa katika kusababisha ugonjwa huu utokee.

    Kutoka kwenye familia yenye historia ya uwepo wa ugonjwa huu, kuwa na uzito mkubwa, umri wa zaidi ya miaka 45, kutokuwa unafanya kazi yoyote pamoja na kuwa na shinikizo la juu la damu na mafuta mengi ni mojawapo ya hali zinazo mhusianisha mtu na kutokea kwa ugonjwa wa kisukari.

    Dalili

    Dalili za kisukari husababishwa na uwepo wa sukari nyingi mwilini ambazo huufanya mwili uanze kuonesha tabia hasi. Baadhi ya dalili hizo ni kuhisi njaa kila mara, kujisaidia haja ndogo mara kwa mara, kuhisi kiu mara kwa mara, kupungua uzito wa mwili, kupatwa na vidonda visivyo pona kirahisi, uchovu wa kila mara bila sababu maalumu, kupungua kwa uwezo wa macho katika kuona, kupungua kwa nguvu za kiume pamoja na hamu ya kushiriki tendo la ndoa.

      Pia, maambukizi ya mara kwa mara ya mfumo wa mkojo, miwasho sehemu za siri na fangasi wa mara kwa mara ni miongoni mwa dalili za ugonjwa huu.

      Kisukari ni mojawapo ya magonjwa yanayoua watu wengi sana duniani kila mwaka.

      Pia, huchangia kwa kiasi kikubwa upofu, magonjwa ya moyo, maambukizi makali, maumivu ya kudumu ya miguu, ugonjwa wa figo, kiharusi, kudumaa kwa afya ya uzazi, kujifungua kabla ya wakati pamoja na kifafa cha ujauzito.

      Tiba

      Matibabu ya kisukari huhusisha mazoezi, lishe, kudhibiti uzito pamoja na matumizi ya dawa.

      Kutokana na aina husika ya kisukari, mhudumu wa afya atatoa dawa pamoja na ushauri wa namna bora ya kutumia dawa hizo.

      Mazoezi husaidia kuunguza nishati pamoja na kupunguza usugu wa mwili katika kutumia vichocheo vya insulin, lakini yanapaswa kufanyika kwa kiasi kwa kuwa wengi huishiwa kabisa sukari wakati huu.

      Ni muhimu kuwa karibu na kifaa cha kupimia sukari wakati wa mazoezi, ili kitoe mwongozo sahihi wa sukari iliyopo mwilini.

      Lishe huchukua sehemu kubwa ya matibabu kwa kuwa karibia kila chakula hugeuzwa kuwa sukari mwilini. Uchaguzi wa vyakula vyenye kiasi kidogo cha mafuta na wanga, nafaka nzima, nyuzi lishe nyingi pamoja na mboga za majani unaweza kuwa chaguo sahihi.

      Ni muhimu kuweka sawa uzito wa mwili. Ukubwa wa athari za kisukari mara nyingi huenda sambamba na kiasi cha uzito alionao mgonjwa. 

      Muhtasari

      Tofauti na miaka ya zamani ambapo vipimo vya ugonjwa huu vilipatikana hospitalini pekee, sasa vipo vya kutosha mtaani.

      Ni muhimu sana kwa kila mtu, lakini zaidi kwa wagonjwa wa kisukari wakiwa na vipimo hivi nyumbani kwao. Itasaidia katika kujua maendeleo yao mara kwa mara kuliko kusubiri hadi hali ibadilike.

      Pia, haishauriwi kuacha kumeza dawa za kisukari hata pale unapoona kuwa hali yako imeimarika pasipo kupata ushauri wa daktari.

      Ugonjwa huu huwa na tabia ya kurudi kwa kasi, hali inayosababisha uwe mgumu katika kuudhibiti.

      Share This Article