Ni vidonge vilivyo tengenezwa kwa homoni mbili zinazofanana na zile zinazopatikana ndani ya mwili wa mwanamke.
Homoni hizo ni huitwa progestin na estrogen
Hufanya kazi kwa kuzuia mwili wa mwanamke usitoe mayai ya uzazi yaliyo pevuka.
Ufanisi
Ufanisi hutegemea na namna mwanamke anameza dawa hizi.
Anayemeza kwa muda sahihi hukinga ujauzito kwa asilimia 97, maana yake katika kila wanawake 100 wanaomeza dawa hizi 97 hukinga ujauzito, watatu hupata ujauzito.
Nafasi ya kutokea kwa ujauzito huwepo kama mwanamke ataanza kumeza dawa siku hizi kwa kuchelewa siku 3 au asipokunywa dawa hizi kwa siku 3 mfululizo.
Faida
Njia hii ni nzuri katika kukinga ujauzito pamoja na aina mbalimbali za saratani zinazosumbua wanawake hasa saratani ya mji wa uzazi pamoja na saratani ya vifuko vya mayai.
Humkinga mwanamke asipatwe na tatizo la upungufu wa damu pamoja na kuvimba vya vifuko vya mayai.
Hupunguza maumivu makali ya hedhi, hedhi zinazobadilika, kuota kwa nywele usoni pamoja na chunusi, maumivu ya nyonga pamoja na maumivu ya ovulation.
Maudhi
Kwa baadhi hubadili mfumo wa hedhi zao kwa kuwafanya wapate hedhi ndogo, hedhi ivurugike au hedhi isiwepo kabisa.
Wengine hupatwa na maumivu ya kichwa, kichefuchefu, kuwasha kwa matiti, hasira za mara kwa mara bila sababu maalumu pamoja na kuongezeka uzito wa mwili.
Kwa baadhi huongeza presha, na namba ndogo sana ya wanawake hupatwa na tatizo la kuganda kwa damu.
Vinamfaa nani?
Karibia kila mwanamke anaweza kutumia njia hii ya uzazi wa mpango. Makundi maalumu ni wanawake walio na watoto tayari, pia ambao bado hawajapata watoto, walioolewa na wasioolewa, baada ya kujifungua na wakati wa kunyonyesha, baada ya kutoa ujauzito, kubaribika kwa ujauzito au kupata ujauzito nje ya mji wa uzazi, wavuta sigara, wenye changamoto za kupungukiwa damu pamoja na wale wenye VVU wanaotumia dawa na wasio tumia dawa.
Nani havimfai?
Baadhi ya makundi ya wanawake hawapaswi kutumia njia hii ikiwemo waliojifungua, wanaoyonyesha na ambao watoto hawajafikia umri wa miezi 6, waliojifungua wiki 3 nyuma lakini hawanyonyeshi, wenye umri wa miaka 35 na zaidi, huku waliwa na tabia ya kuvuta sigara pamoja na wenye miaka 35 na zaidi huku wakiwa na changamoto ya kuugua kipanda uso mara kwa mara.
Pia, wenye shinikizo la juu la damu, kisukari, wanaotumia baadhi ya dawa mfano lamotrigine, carbamazepine na primidone ambazo hupunguza ufanisi wa njia hii ya uzazi wa mpango pamoja na wanawake mwenye ujauzito tayari.
Masharti ya kumeza
Karibia kila mwanamke asiye na ujauzito kwa wakati huo anaweza kumeza vidonge hivi
Kama alikuwa anatumia kalenda
Kama mwanamke atameza kuanzia siku ya 5 ya hedhi yake, atakingwa kwa asilimia 100 dhidi ya ujauzito.
Kama ataanza kumeza kuanzia siku ya 6 na kuendelea, atahitajika kutumia njia nyingine ya kukinga ujauzito ndani ya siku 7 za matumizi ya dawa hizi kwa kuwa hatokuwa amepata kinga kamili.
Kama alikuwa anatumia sindano, au dawa zingine
Anaweza kuanza kumeza moja kwa moja baada ya kuachana na njia husika. Hakuna haja ya kusubiria hedhi, atapata kinga ya kuzuia ujauzito moja kwa moja
Kama ananyonyesha kwa asilimia 100
Inafaa kusubiri hadi miezi 6 ipite, wakati ambao mtoto atakuwa anatumia pia vyakula mbadala
Kama mama kafikisha zaidi ya miezi 6 ananyonyesha na hedhi haijarudi, ataanza kunywa dawa muda wowote lakini ndani ya siku 7 za matumizi ya dawa itafaa atumie njia mbadala kujikinga kwa sababu anaweza kupata ujauzito. Ikiwa hedhi imerudi, atameza kuanzia siku ya 5 ya mzunguko.
Wanaonyonyesha kidogo
Anapaswa kuanza kumeza kuanzia wiki ya 6 baada ya kujifungua. Ikiwa hedhi itakuwa imerudi, atapaswa kuanza kumeza kuanzia siku ya 5 ya hedhi yake ili kupata ulinzi kamili
Wasionyonyesha kabisa
Anaweza kuanza siku yoyote kati ya 21 – 28 tangu ajifungue.
Ikiwa ataanza kumeza baada ya mwezi wa kwanza tangu ajifungue, atameza siku yoyote lakini siku 7 za kwanza lazima atumie njia nyingine ya uzazi wa mpango ili kujilinda.
Ikiwa hedhi itakuwa imerejea, anashauriwa kumeza kuanzia siku ya 5 ya hedhi kama yalivyo makundi mengine.
Asiyepata kabisa hedhi
Anaweza kumeza siku yoyote, lakini siku 7 za kwanza atapaswa kuwa makini kwa kutumia njia mbadala kujikinga na ujauzito.
Aliyetoa ujauzito au ambaye ujauzito umeharibika
Anaweza kumeza moja kwa moja baada ya tukio hili.
Ikiwa atameza baada ya siku 7 tangu tukio husika litokee, atapaswa kutumia njia mbadala kujilinda siku 7 za mwanzo ili asipate ujauzito.
Mfumo wa vidonge
Kuna aina nyingi za vidonge hivi lakini aina mbili maarufu sana ni zile za tembe 28 na 21.
Zile zilizofungwa 28 kwa pamoja huwa na vidonge 21 vyenye vichocheo, huku vidonge 7 vyenye rangi tofauti vikiwa havina vichocheo. Hali kadhalika, ambavyo huwa 21 kwa pamoja vyote huwa na vichocheo.
Ikiwa mwanamke atapatiwa vidonge 28, atapaswa kumeza kila siku hadi pale ambapo seti ya kifungashio cha kwanza kitaisha, kisha ataendelea na kifungashio kingine siku inayofuata.
Ikiwa mwanamke atapatiwa vidonge 21, atapaswa kuvimeza vyote kwa siku 21 mfululizo, kisha atasubiria kwa siku 7 ndipo afungue kifungashio kingine
Muhtasari
Ni muhimu kujenga utaratibu wa kumeza dawa hizi muda uleule kila siku ili kupunguza maudhi yake, pamoja na kusaidia kurekebisha changamoto mbalimbali za mwili.
Kutokwa na matone madogo ya damu, kubadilika kwa hedhi au kutokuonekana kabisa kwa hedhi ni mambo ya kawaida kuonekana wakati wa matumizi ya majira.