Faida za Usingizi kwa Afya

4 Min Read

Usingizi ni jambo la asili linalohusisha utulivu wa akili na mwili kwa ujumla, wakati ambao macho hufumba na ufahamu huondoka ili kupunguza miondoko ya mwili hasa katika kujibu vichocheo vya nje.

Usingizi ni jambo la muhimu kwa afya ya binadamu, huufanya mwili wa binadamu upitie mambo ya kustaajabisha sana wakati huu.

Mtu akisema wanasayansi hawajui kwanini binadamu hulala atakuwa ni muongo.

Tunalaa ili tuishi, kama ambavyo chakula ni muhimu kwa mwili wa binadamu, hali ipo hivyo pia kwa usingizi. Usipokula utakufa, hali kadhalika usipolala utakufa.

Zifuatazo ni faida za usingizi kwa afya;

1. Ubongo

Kabla ya mwaka 2015, wanasayansi waliamini kuwa mwili huwa na mfumo mmoja tu wa kukusanya na kutoa uchafu mwilini, maarufu kama mfumo wa lymphatic.

Inakuwaje ubongo ulio mwalimu wa matendi yote ya mwili ukose mfumo wa kutoa taka zake?

Watafiti Antonie Louveau na Aleksanteri waligundua kuwa ubongo unao mfumo maalumu wa kutoa taka unaoitwa mfumo wa glymphatic.

Huhusika katika kutoa taka za protini zinazoitwa amyloid beta ambazo hujikusanya kwenye ubongo. Taka hizi huhusishwa na magonjwa mengi ya akili.

Mfumo huu hufanya kazi vizuri tuwapo usingizini. Mtu asipolala taka za amyloid beta hujikusanya na kuathiri ubongo. (1,2)

Kadri usivyolala muda mrefu ndivyo taka zinavyozidi kuwa nyingi hivyo kuulemaza ubongo, pamoja na namna unavyofanya kazi.

2. Uzito

Kutokulala husababisha ongezeko kubwa la uzito kupitia nadharia nne zinaoelezwa kisayansi.

Nadharia ya kwanza ni kuwa mtu asipolala vichocheo vya njaa vinavyoitwa ghrelin huzalishwa kwa wingi hivyo kuongeza pia nafasi ya kula mara kwa mara na kuongezeka uzito.

Pili, leptin ni kemikali inayoufanya mwili ujisikie umeshiba pamoja na kuupunguzia hamu ya kula kabla ya njaa.

Uzalishwaji wa kemikali hizi hupungua sana pale mtu asipolala hivyo kumfanya mhusika ale mara kwa mara.

Tatu, upungufu wa usingizi huufanya mwili upungukiwe na akiba ya nishati na ili uweze kuzirejesha, ni lazima mtu ale sana.

Usingizi hafifu hupunguza ufanisi wa mwili katika kudhibiti hisia zake. Hii inaweza kuzaa tabia ya kutokuwajibika kwenye kula. (3,4,5,6)

Nafikiri umeona uhusiano wake.

3. Mihemko

Ukosefu wa usingizi unaweza kusababisha sonona, wasiwasi pamoja na mawazo hasi kwenye ubongo.

Baadhi ya madaktari huwa hawawezi kutoa majibu ya uwepo wa sonona kwa mgonjwa pasipo kuonesha dalili za kukosa usingizi. (7)

4. Saratani

Kuna tafiti nyingi zinazofafanua uhusiano wa kutokulala na kuugua saratani mbalimbali hasa tezi dume, kinywa, utumbo mkubwa pamoja na mfumo wa neva za fahamu.

Kwa tafiti za sasa, kuha uhusiano mkubwa kati ya kutokulala na kuugua saratani ya matiti. (8)

5. Kinga

Mfumo wa kinga za mwili hutegemea kwa kiasi kikubwa ubora wa usingizi.

Mfano, Mwaka 2015 Mtafiti Aric Prather kutoka chuo kikuu cha California aliwapa watu aina moja ya virusi inayoitwa rhinovirus ambaye husababisha maambukizi kwenye sehemu ya juu ya mfumo wa hewa. (9)

Watu waliopewa kirusi huyu kisha wakala muda mchache waliugua kwa kiasi kikubwa kuliko wale waliopewa kisha wakalala kwa muda mrefu.

Muhtasari

Kuna taarifa nyingi zinazo kinzana kuhusu muda sahihi wa masaa ya kulala.

Kwa maoni yangu, binadamu anapaswa kulala kwa masaa yoyote anayoona kwake akiamka hatapata shida ya kujisikia bado anao usingizi mwingi.

Wastani wa masaa 8 unaweza kuwa mzuri kwa mtu mzima.

Muda huu unaweza kuongezeka zaidi kwa watoto ili kuruhusu ukuaji bora.

Share This Article