Chanzo cha UTI Sugu kwa Wanawake

5 Min Read

Ugonjwa wa UTI ni maambukizi kwenye sehemu yoyote inayounda mfumo wa mkojo. 

Walau mwanamke mmoja katika kila kundi la wanawake watano huwa na tatizo la kujirudia la UTI.

Wanaume pia wanaweza kuwa na changamoto hii, lakini kwao huwa ni ngumu sana kutokea tofauti na wanawake.

Sababu za Kujirudia

Tofauti za kimaumbile pamoja na mtindo wa maisha huchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa tatizo la UTI inayo jirudia mara kwa mara.

1. Maumbile

Maumbile ya wanawake yapo tofauti sana na wanaume.

Huwa na mrija mfupi wa mkojo, pia tundu la uke na tundu la sehemu ya haja kubwa huwa vipo karibu sana.

Hii inatoa maana kuwa ni rahisi sana kwa bakteria wanaosababisha ugonjwa huu kutoka kwenye sehemu ya haja kubwa kuingia ukeni, kisha wakawa na muda mfupi sana wa kusafiri ndani ya mfumo kwa kuwa mrija ni mfupi. (1)

Hii hurahisisha maambukizi ya UTI na kuifanya irudie mara kwa mara.

2. Usafi

Kwa kuwa mrija wa mkojo ni mfupi sana, na tundu la uke lipo karibu na tundu la sehemu ya haja kubwa, ni rahisi sana kwa choo kuingia ukeni wakati wa kujisafisha.

Kwa mantiki hii, mwanamke hushauriwa kujisafisha kutoka mbele kwenda nyuma, yaani kutoka sehemu lilipo tundu la uke kuelekea sehemu ya haja kubwa. (2,3)

Hii itaondoa nafasi ya kuingia kwa choo na uchafu mwingine kwenye uke.

3. Ngono

Bakteria wanaosababisha ugonjwa wa UTI wanaweza kusambaa kirahisi wakati wa ngono kutoka kwa mwanamme, vidole, ulimi au pia kutoka kwenye vifaa vya ngono (sex toys).

Msuguano huo unaweza kuwa chanzo cha kuambukizwa kwa UTI.

Hata hivyo, ni vizuri kufahamu kuwa UTI siyo ugonjwa wa zinaa, isipokuwa mazingira ya ufanyikaji wa tendo hili unaweza kurahisisha uambukizwaji.

Hushauriwa kwenda haja ndogo kila baada ya kushiriki ngono ili kuwaondoa bakteria wabaya kwenye mrija wa mkojo, ikiwa watakuwa wameingia.

4. Maji

Kutokunywa maji ya kutosha inaweza kusababisha kutokea kwa ugonjwa huu. Unywaji wa maji mengi husaidia kuondoa bakteria wabaya kwenye mfumo wa mkojo. 

Tafiti nyingi zinaelezea kuwa wanawake wanaokunywa maji mengi huwa na uwezekano mdogo wa kupatwa na tatizo hili mara kwa mara. (4,5)

Kunywa walau lita 2.5 hufaa kwa siku.

5. Unyevu

Unyevu huwa ni mazingira mazuri ya kuzaliana kwa bakteria na vimelea vingine vya magonjwa.

Inashauriwa mwanamke avae nguo zilizo tengenezwa kwa pamba asilimia mia moja kwa kuwa huwa na sifa ya kufyonza unyevu. (6)

Pia, ni muhimu kuvaa nguo za ndani zilizokauka, pamoja na kujikausha kwanza vizuri kabla ya kuvaa nguo za ndani.

6. Tabia Hatarishi

Kubana mkojo kwa muda mrefu ni tabia hatarishi inayosababisha tatizo la kujirudia la ugonjwa wa UTI. Kadri mkojo unavyobanwa ndivyo bakteria wanavyozaliana.

Tabia ya kudeki uke, yaani kutumia kemikali kama vinegar, magadi pamoja na kemikali zingine kali huathiri mazingira ya asili ya uke hivyo kukaribisha maambukizi ya mara kwa mara.

7. Magonjwa

Magonjwa kama kisukari na mawe kwenye figo huchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa ugonjwa wa UTI isiyotibika kirahisi.

Magonjwa haya hutengeneza mazingira rafiki ya kuzaliana kwa vimelea vya magonjwa. (8, 9)

Kwa kuwa kinga ya mwili hasa kwenye maeneo hayo huwa imeshuka pia, ni rahisi sana kwa maambukizi kutokea.

8. Ujauzito

Mkojo wa mwanamke mjamzito huwa na kiasi kikubwa cha vichocheo vya mwili, sukari na protini.

Pia, mji wa uzazi hutengeneza mgandamizo mkubwa kwenye kibofu cha mkojo hivyo kukifanya kishindwe kutoa mkojo wote wakati wa haja ndogo. (10)

Jambo hili hubakiza masalia ya mkojo, pamoja na bakteria wabaya ambao huzaliana na kusababisha UTI ya mara kwa mara.

9. Usugu

Kama ambavyo binadamu hapendi kufa, hali hii ipo hivyo pia kwa vimelea vya magonjwa. 

Kadri tunavyotumia dawa pasipo kufuata ushauri sahihi wa wahudumu wa afya pamoja na kujiamlia wenyewe aina ya dawa ya kunywa pasipo hata kupima, vijidudu hutengeneza mbinu na mifumo mipya ya kujilinda na dawa hizi.

Vijidudu hugeuka kuwa sugu, na huwa haviwezi tena kudhurika na kufa hata baada ya kumeza dozi sahihi. (11,12)

Pengine hauponi ugonjwa huu kwa kuwa vimelea vyako vimeshakuwa sugu.

Muhtasari

Hata kama umehangaika sana kufuata aina mbalimbali za tiba pasipo mafanikio, bado nafasi ya kupona kabisa ugonjwa huu ipo.

Fika hospitalini uchunguzwe tena. Utatibiwa.

Share This Article