Ugonjwa wa UTI: Dalili, Kinga na Tiba

5 Min Read

UTI ni ufupisho wa maneno Urinary Tract Infection, au kwa kiswahili ikiwa ni maambukizi ya sehemu yoyote ya mfumo wa mkojo ambao huhusisha figo, kibofu cha mkojo, mrija wa mkojo pamoja na mrija unaounganisha figo na kibofu cha mkojo.

Maambukizi haya kwa kiasi kikubwa husababishwa na bakteria jamii ya E. coli, lakini katika mazingira machache fangasi na virusi wanaweza kuwa chanzo cha maambukizi haya.

Maambukizi ya mfumo wa mkojo yanaweza kugawanywa kwenye makundi mawili yaani maambukizi ya sehemu ya chini ya mfumo, yakihusisha mrija wa mkojo na kibofu cha mkojo au maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo yakihusisha figo au mrija unaounganisha figo na kibofu.

Maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo huwa ni machache ikilinganishwa na maambukizi ya sehemu ya chini ya mfumo.

Huwa pia na dalili na madhara makubwa zaidi.

Dalili

Maambukizi ya sehemu ya chini ya mfumo huwa na dalili za kupatwa na maumivu wakati wa haja ndogo, kupatwa haja ndogo mara kwa mara isiyotoa mkojo mwingi, mkojo mweusi au ulio na chembechembe za damu, harufu kali pamoja na maumivu ya sehemu ya haja kubwa kwa wanaume au nyonga kwa wanawake.

Maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo huambatana na homa, kutapika, maumivu nyuma ya mgongo na kiungulia.

Wanawake

Wanawake huwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuugua ugonjwa huu kutokana na ukweli kuwa mrija wao wa mkojo huwa ni mfupi sana, pia tundu la uke huwa karibu na sehemu ya haja kubwa.

Ni rahisi kwa bakteria kutoka kwenye choo kuingia ukeni.

Matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango, matumizi ya kondomu, matumizi ya kemikali kali kusafishia uke hasa zile zenye lengo la kuua mbegu za kiume, kufikia umri wa ukomo wa hedhi, ushiriki wa tendo la ndoa ambao huweka msuguano mkubwa unaoweza kuingiza bakteria kutoka kwenye tundu la haja kubwa pamoja na ujauzito ambao hubana kibofu cha mkojo huwa ni baadhi ya sababu zinazoongeza uwezekano wa wanawake kuugua ugonjwa huu kuliko wanaume.

Umeelewa sasa kwanini wanawake huugua kirahisi ugonjwa huu kuliko wanaume?

Wanaume

Wanaume wenye changamoto zozote zile zinazohusisha tezi dume huwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kuugua ugonjwa huu kuliko wanaume walio salama.

Hata hivyo, jinsia hii sio wahanga wakubwa wa UTI kama ilivyo wanawake.

Visababishi Vingine

Kuwekewa mrija wa mkojo, mawe kwenye figo, uzee na uwepo wa upungufu wa kinga za mwili ni vababishi vinavyoongoza katika kuongeza nafasi ya kutokea kwa tatizo hili.

Uwepo wa baadhi ya magonjwa kama kisukari huwa pia ni kisababishi kingine kikubwa.

Tiba

Mhudumu wa afya hutoa dawa kulingana na uhakika alio upata kutok kwenye majibu ya vipimo.

Matibabu ya UTI huhusisha matumizi ya dawa za viua vijasumu (antibayotiki) mfano amoxicillin, ceftriaxone na amoxclav.

Aina zingine pia za matibabu zinaweza kuchaguliwa kadri itakavyoonekana inafaa.

Kinga

Kuna baadhi ya njia zinazoweza kutumika kujikinga na tatizo la UTI. Mfano wa njia hizi ni kunywa walau lita 2 za maji kila siku, kutokuvaa nguo za ndani zinazobana sana, kuvaa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa pamba asilimia 100 pamoja na Kutumia juisi za matunda mara kwa mara.

Pia, kuacha mazoea ya kuvaa nguo za ndani mbichi, kujisafisha kutoka mbele kwenda nyuma ili kuzuia bakteria wasiingie kwenye uke kutoka shimo la haja kubwa, kwenda haja ndogo kila baada ya kushiriki tendo la ndoa, kuacha tabia ya kutunza mkojo baada ya kuhisi haja ndogo na kutokushiriki mapenzi kinyume cha maumbile ni miongoni mwa njia zinazoweza kusaidia kujikinga na ugonjwa huu.

    Muhtasari

    Wanawake huwa na asilimia 30 zaidi ya kupata tatizo la UTI kuliko wanaume.

    Hata hivyo, maambukizi haya kwa jinsia zote ni ya kawaida.

    Unapohisi dalili za uwepo wa maambukizi haya fika hospitalini uchunguzwe na kutibiwa.

    Share This Article