Athari za Maziwa ya Ng’ombe kwa Watoto chini ya Mwaka Mmoja

2 Min Read

Maziwa ya ng’ombe ni mojawapo ya chakula kilicho na virutubisho vingi vinavyofaa kwa afya ya binadamu.

Pamoja na ubora wake huu, aina hii ya maziwa haifai kwa mtoto mwenye umri chini ya mwaka mmoja.

Sababu

Kwanza, huwa na kiasi kidogo sana cha madini chuma yasiyokidhi mahitaji ya mtoto ambae hukua kwa kasi wakati huo, hivyo kuyategemea sana kunaweza kusababisha mtoto apatwe na changamoto ya upungufu mara kwa mara wa damu.

Pia, Wastani wa asilimia 40 ya watoto chini ya mwaka mmoja wanaotumia maziwa ya ng’ombe hupatwa na tatizo la kuvujia kwa damu kwenye utumbo hivyo kuwafanya wapoteze damu nyingi kupitia choo.

Aidha, huwa na kiasi kikubwa sana cha protini pamoja na madini ambavyo kwa umri wake huwa ni ngumu sana kuvitunza mwilini. Kiasi cha ziada hupaswa kutolewa kupitia mkojo, hivyo ni lazima mwili wa mtoto upoteze pia maji mengi katika kutoa nje uchafu huu.

Kuna taarifa za uhakika kuwa watoto wanaopatiwa maziwa ya ng’ombe kwenye umri huu hukabiliwa mara kwa mara na tatizo la upungufu mkubwa wa maji mwilini.

Maziwa haya ni mazuri kwa afya. Yanapaswa kutolewa kwa mtoto baada ya kufikia mwaka mmoja na siyo chini ya hapo.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, athari hizi hupungua kadri umri wa mtoto unavyozidi kuwa mkubwa.

Ushauri

Mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaelekeza kuwa mtoto anapaswa kutumia maziwa ya mama pekee kwa kipindi chote cha miezi 6 ya mwanzo, pasipo kupatiwa hata maji ya ziada kwa kuwa sehemu kubwa ya maziwa huundawa maji.

Baada ya hapo, mtoto anaweza kupatiwa vyakula vya nyongeza huku akiendelea kunyonya maziwa ya mama.

Ikiwa kutakuwa na uhitaji mkubwa wa kupatiwa maziwa ya ziada, ni muhimu apewe maziwa ya kopo maarufu kama fomula.

Share This Article