Vyakula Muhimu kwa Mtoto Baada ya Kutimiza Miezi 6

4 Min Read

Upungufu wa virutubisho ni tatizo kubwa lililopo duniani.

Watoto, wanawake wajawazito na wazee ni makundi matatu makubwa yaliyo kwenye hatari kubwa ya kupatwa na tatizo hili.

Upungufu huu unaweza kusababishwa na ulaji wa mlo duni, uwepo wa hitilafu mwilini katika kumeng’enya chakula pamoja na kufyonza virutubisho, uwepo wa magonjwa yanayoufanya mwili upoteze virutubisho vingi mfano kuhara pamoja na kuongezeka kwa uhitaji wa virutubisho mwilini kutokana na hali ya afya ya wakati ule. (1,2)

Watoto ni kundi linalohitaji nishati na virutubisho muhimu kwa ajili ya ukuaji na kujitegemea.

Hivi ni baadhi ya virutubisho muhimu vinavyopaswa kuongezwa kwenye mlo wa mtoto baada ya kufikisha miezi 6.

1. Vitamini K

Kwa kuwa vitamini K haiwezi kupita kondo la uzazi, watoto hukabiliwa na upungufu mkubwa wa vitamini hii hivyo huchomwa sindano yenye vitamini K ndani ya saa 1 baada ya kuzaliwa ili kuwakinga na tatizo la kupoteza damu nyingi pamoja na kifo. (3,4)

Vitamini K huhusika moja kwa moja katika kugandisha damu mwilini.

Unaweza kuipata kwa wingi kwenye mboga za majani.

2. Vitamini D

Watoto wanapaswa pia kupewa virutubisho vya vitamini D kwa kuwa maziwa ya mama huwa na kiasi kidogo cha vitamini hii. (5,6)

Husaidia katika kuufanya mwili utunze madini ya calcium na phosphorous, pia ni muhimu katika utengenezwaji wa mifupa.

Unaweza kuipata kutoka kwenye samaki, kiini cha mayai, uyoga pamoja na maziwa ya ng’ombe.

Hata hivyo, maziwa ya ng’ombe huwa na virutubisho vingi ambavyo mtoto hawezi kuvimeng’enya, huwa na kiasi kidogo cha madini ya chuma hivyo kuongeza hatari ya kutokea kwa upungufu wa damu kwa mtoto, huwafanya wapoteze damu na maji mengi pamoja na kupata mzio. (7)

Mtoto mwenye umri wa chini ya mwaka mmoja hapaswi kupewa maziwa ya ng’ombe.

3. Vitamini B12

Kwa mama asiyekula nyama, mtoto anaweza kukabiliwa na upungufu wa vitamini B12. Hii ni vitamini muhimu sana katika kutengeneza damu pamoja na vinasaba vya mwili. 

Mama mjamzito anashauriwa kula nyama, maziwa na mayai ili kumkinga mtoto na athari za kiafya, ikiwa ni pamoja na udumavu wa akili.

Mtoto apatiwe pia virutubisho hivi kwenye mlo wake, baada ya kufikisha miezi 6.

4. Protini

Tatizo kubwa lililopo kwenye jamii yetu ni kuwapatia watoto vyakula vingi vyenye wanga kuliko protini ambayo ndiyo kiini cha ukuaji wao.

Kwa kiasi kikubwa, upungufu wa virutubisho unaotokea kwa wingi ni ule unaohusisha protini hivyo kuongeza unyafuzi na udumavu kwa watoto. (8)

Ni muhimu kwa wazazi kubadili mlo kwa kuwapa watoto wao samaki, mbegu za maboga, mayai, vyakula jamii ya karanga na nyama

Nyongeza

Upungufu wa madini ya copper, zinc, chuma, asidi ya foliki pamoja na vitamini A na vitamini C huathiri pia ukuaji wa kimwili na kiakili kwa watoto.

Ubadilishaji wa mlo unaojumlisha matunda, mboga za majani, nyama, samaki, mafuta pamoja na nyuzilishe husaidia katika kuboresha afya ya mtoto, pia kuwakinga dhidi ya magonjwa ya mara kwa mara. (9,10)

Ni muhimu kwa wazazi kutokutegemea unga wa lishe pekee maana hauwezi kukidhi uhitaji mkubwa wa virutubisho kwa mtoto.

Share This Article