Karafuu: Virutubisho na Faida kwa Afya

5 Min Read

Kitaalamu huitwa Syzygium aromaticum, na hupatikana kwenye familia kubwa inayoitwa Myrtaceae.

Ili karafuu iweze kutambulika kuwa halali, isiyochakachuliwa, hupaswa kuwa na kiasi cha mafuta yake yanayoitwa eugenol si chini ya walau asilimia 70 ya uzito wake ikiwa imekaushwa.

Hupatikana sehemu nyingi duniani ikiwemo Zanzibar, Madagascar, Sri Lanka na India na huanza kutoa matunda yake baada kufikia wastani wa miaka 7 hadi 8, au zaidi ya hapo.

Virutubisho

Karafuu huwa na viondoa sumu, nyuzi lishe, vitamini K, manganese, vitamini C, kiasi kidogo cha vitamini E, calcium na magnesium.

Sehemu kubwa inayobaki hubebwa na maduta yake maalum yanayoitwa eugenol ambayo ndio huzipa karafuu sifa nyingi za kutumika kama dawa na viungo vya chakula.

Karafuu huwa na faida nyingi kwa afya ya binadamu, baadhi yake ni hizi;

1. Meno

Mafuta ya eugenol yanayopatikana kwenye karafuu huwa na sifa ya kutuliza maumivu na kuondoa uvimbe.

Ni tiba iliyoanza kutumika tangu karne ya 19.

Huko mwanzo, mafuta haya yalitumika moja kwa moja katika kutengeza dawa za kuzibia meno kwa wagonjwa, pamoja na kusaidia watu wote wenye changamoto za meno. (1,2,3)

Leo pia mafuta haya yanaweza kutumika kwa kazi hii.

2. Gesi

Kama unasumbuliwa na tumbo kujaa gesi mara kwa mara, sasa umepata suluhisho.

Huongeza ufanisi wa mfumo wa chakula katika kumenge’enya na kuzalisha vimeng’enya vinavyohitajika kwa wakati sahihi. (4,5)

Inaweza kutumika kwa kutafuna, pia kama kiungo cha chakula.

Ifanye sasa kuwa rafiki wa jiko lako.

3. Vidonda vya Tumbo

Karafuu husaidia kulinda kuta za tumbo ili zisichimbike.

Aina nyingi za vidonda vya tumbo husababishwa na kuliwa kwa ukuta wa tumbo wenye ute ambao husimama kama kinga.

Karafuu huongeza uzalishwaji wa ute huu pamoja na kuweka mazingira rafiki kwenye kuta za tumbo, huchangia kuongezeka kwa ulinzi, hivyo kukinga dhidi ya vidonda vya tumbo. (6,7,8)

Ni tiba nzuri ya mbadala katika kutibu tatizo la vidonda vya tumbo.

4. Chakula

Unawezaje kula chakula chako pasipo kuweka karafuu hasa ukiwa Zanzibar? Ni ngumu kukuta, na inaweza isiwepo kabisa.

Tangu karne za kale, karafuu imekuwa inatumika kama kiungo muhimu sana kwenye kuongeza ladha ya chakula.

Harufu yake ya kuvutia, pamoja na ladha yake isiyo kifani huchochea wapishi wengi kuijumlisha kwenye sufuria zao.

5. Vimelea

Tafiti kadhaa zimefafanua uwezo wa karafuu katika kupambana na vijidudu vya magonjwa hasa bakteria. (9)

Hufanya kazi kwa kudhibiti ukuaji wao, hivyo kuongeza usalama wa afya ya mhusika.

6. Saratani

Japo hakuna tafiti za kutosha zilizofanyika kwa binadamu, kemikali zinazopatikana kwenye karafuu zinatajwa kuwa na uwezo wa kukinga pamoja na kupambana na aina mbalimbali za saratani. (10,11)

Tafiti hizi zinapaswa kufanywa kwa binadamu ili kutoa uhakika wa kazi hii.

7. Sumu

Uwepo wa vitamini C na madini mbalimbali huifanya karafuu kuwa na sifa nzuri ya kuondoa sumu mwilini.

Tabia hii humsaidia binadamu awe na kinga thabiti ya kupambana na magonjwa sugu.

Matumizi ya mara kwa mara ya karafuu pamoja na vyakula vingine vyenye vitamini C kutauandaa mwili kikamilifu katika kupambana na maradhi. (12)

Usiishie kula limao na chungwa pekee, tumia pia karafuu itakusaidia.

8. Uvimbe

Huwa na kampaundi nyingi zinazopambana na  aina mbalimbali za uvimbe mwilini.

Eugenol imeelezwa na tafiti kuwa na uwezo wa kudhibiti viamsho vya uvimbe pamoja na kupunguza maumivu ya sehemu hizi.

Tafiti kadhaa zinakazia kazi hii hasa kwenye mapafu. (13,14)

Unajua kuwa mapafu hufanya kazi kama lilivyo puto la hewa? Yalinde.

9. Ngozi

Unataka kuboresha muonekano wa ngozi yako?

Karafuu hufaa kwenye kushughulikia changamoto mbalimbali za ngozi hasa chunusi na mabaka.

Huondoa pia makunyazi pamoja na kuondoa michubuko hasa ile inayosababishwa na jua, matumizi ya vipodozi pamoja na ajali. Kama wewe ni mdau wa urembo huwezi kupuuzia matumizi ya mafuta ya mmea huu.

Muhtasari

Unasubiri nini kuanza kutumia karafuu?

Ni bidhaa inayopatikana kwa urahisi kwenye maeneo mengi. Husaidia pia kuondoa changamoto za kinywa kutoa harufu mbaya.

Itafute ikusaidie sasa.

Share This Article