Ukiambiwa kutaja bidhaa moja inayoweza kutunzwa kwa miaka mingi pasipo kuharibika hauwezi kuikwepa asali.
Ni chakula kitamu ambacho hulinganishwa na ladha ya mapenzi.
Historia ya chakula hiki imedumu kwa karne nyingi, kuanzia enzi za mababu zetu hadi sasa.
Virutubisho
Viambato viwili vikubwa vya asali ni maji na sukari.
Kwa mujibu wa Idara ya Chakula ya Marekani (USDA), asali huwa pia na amino acids, protini, viondoa sumu, vitamini mbalimbali pamoja na madini chuma, sodium, zinc, potassium, copper, selenim, fluoride na calcium.
Faida za asali ni hizi;
1. Sumu
Asali huwa na viondoa sumu vingi ambavyo huuhakikishia mwili usalama, pamoja na kuongeza kinga yake.
Sumu hizi ni hatari, zinaweza kusababisha magonjwa kama kisukari, magonjwa ya moyo pamoja na kuzeeka mapema.
Ulaji wa asali hutoa uhakika wa kuziondoa, hivyo kuuacha mwili ukiwa salama. (2,3,4)
Pamoja na kusababisha magonjwa sugu, huua pia seli za mwili ambazo ni kitovu cha uhai wa binadamu.
2. Vidonda
Asali hutumika kutibu vidonda vya aina mbalimbali.
Hii inatokana na sifa yake ya kuwa na uwezo wa kupambana na aina mbalimbali za vimelea vya magonjwa pamoja na kuzuia uvimbe.
Inaweza pia kutumika katika kutibu changamoto zingine za magonjwa ya ngozi. (5)
Hutumika kwa kupaka sehemu ya kidonda baada ya kukisafisha.
3. Kikohozi
Asali hufanya kazi kama zilivyo syrup za kutibu kikohozi. Ni dawa nzuri sana kwa watoto wenye umri wa zaidi ya mwaka mmoja pamoja na watu wazima.
Tafiti kadhaa zinaelezea kuwa, asali ikitumika vizuri inaweza kuwa tiba ya haraka zaidi ya kikohozi kuliko hata dawa za hospitalini. (6,7)
Unasumbuliwa na kikohozi cha mara kwa mara? Tumia asali.
4. Uzazi
Hauwezi kusimulia kazi za asali pasipo kutaja sifa ya kusaidia uboreshaji wa afya ya uzazi.
Husaidia kutatua changamoto ya upungufu wa nguvu za kiume, uzalishaji wa mbegu dhaifu pamoja na kusaidia wanawake wenye changamoto za ugumba hasa zitokanazo na mapungufu mbalimbali yanayohusu mzunguko wa hedhi. (8,9)
Njia nyingine za kupata ujauzito kirahisi unaweza kuzisoma hapa.
5. Vimelea
Afya ya binadamu huwekwa rehani baada ya kushambuliwa na vimelea vya magonjwa.
Hawa ni wageni wabaya wanao ingia mwilini pasipo idhini, kisha husababisha aina mbalimbali za magonjwa.
Tafiti zinabainisha uwezo wa asali kwenye kupambana na aina mbalimbali za vimelea vya magonjwa hasa bakteria na fangasi. (9,10,11)
Ni muhimu ukiitumia mara kwa mara.
6. Mfumo wa Chakula
Asali husaidia kutibu vidonda vya tumbo.
Unajua kwanini?
Mojawapo ya sababu za kutokea kwa vidonda vya tumbo ni uwepo wa maambukizi ya vimelea vya bakteria jamii ya H. pylori ambao asali huwa na uwezo wa kuwaangamiza.
Aidha, hutibu pia tatizo la kuhara pamoja na kuboresha mazingira ya ukuaji wa bakteria wazuri wanaohitajika tumboni. (12)
Tumia asali kila siku ili ikupe faida hizi.
7. Urembo
Asali husaidia kwenye kutibu tatizo la chunusi.
Husaidia kufungua vinyweleo vya ngozi, kuongeza ubichi wa ngozi pamoja na kuongeza uangavu wake. (13)
Hufaa zaidi kama asali itachanganywa pamoja na unga wa mdalasini ili kuleta majibu mazuri zaidi.
8. Ubongo
Huboresha afya ya ubongo.
Kwa namna ya kipekee kabisa, asali huongeza uwezo wa ubongo kwenye kuchakata taarifa, kujifunza, kufikiri na kutunza kumbukumbu.
Hutoa kinga dhidi ya magonjwa ya akili yanayosababishwa na uzee
9. Nishati
Umefanya kazi ngumu kwa siku nzima na unahisi uchovu?
Asali ni chanzo bora sana cha nishati. Kwa mujibu wa Idara ya Chakula ya Marekani (USDA), gramu 100 za asali hutosha kukupa nishati 304 kcal.
Kijiko kimoja cha mezani kinatosha kabisa kukupa 64 calories. Itumie kukuongezea nguvu.
Tahadhari
Asali haifai kutolewa kwa watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja kwa kuwa mfumo wao wa kinga, pamoja na ule wa chakula huwa haujakomaa vizuri.
Asali huwa na asilimia kubwa ya kubeba bakteria wabaya jamii ya Clostridium botulinum ambao kwa umri huo, mtoto huwa hawezi kuwaharibu akiwala.
Husababisha tatizo hatari lisilo onekana mara kwa mara linaloitwa Infant botulism ambalo huwa na dalili za choo kigumu, kuweweseka, kifafa, changamoto za kupumua na hatimaye kifo ikiwa msaada wa haraka hautatolewa.
Watoto wenye zaidi ya mwaka mmoja, watu wazima, wanawake wajawazito pamoja na wazee wanaweza kutumia asali kwani miili yao huwa imekomaa vya kutosha kupambana na bakteria hawa.