Karoti: Virutubisho, Faida na Tahadhari kwa Afya

6 Min Read

Karoti kwa kisayansi hujulikana kama Daucus carota.

Ni chakula chenye asili ya mzizi kilichoanza kulimwa tangu kale.

Karoti hupatikana ikiwa kwenye mfumo wa rangi mbalimbali mfano zambarau, njano, nyekundu pamoja na rangi nyeupe.

Virutubisho

Karoti huwa na protini, wanga, nyuzilishe, sukari, madini chuma, calcium, phosphorus, sodium, zinc, manganese, copper, fluoride na vitamini C.

Pia, mzizi huu huwa na kiasi kikubwa cha maji, aina mbalimbali za vitamini B, choline na viondoa sumu.

Mjumuiko huu wa virutubisho umeorodheshwa hapa kwa kufuata rejea za Idara ya Chakula ya Marekani USDA.

Karoti husaidia sana katika kuboresha afya ya binadamu. Baadhi ya kazi za karoti zimeainishwa hapa chini.

1. Macho

Karoti huwa na kiasi kikubwa cha kemikali zinazoitwa beta carotene ambazo hubadilishwa ndani ya mwili wa binadamu kuwa vitamini A.

Virutubisho hivi husaidia kuboresha afya ya macho kwa kuongeza uoni, pamoja na kuzuia magonjwa mbalimbali ya macho ambayo huhusishwa moja kwa moja na kusababisha tatizo la upofu.

Boresha afya ya macho kwa kutumia karoti.

2. Damu

Vitamini K1 inayopatikana kwenye karoti husaidia kurahisisha zoezi la kuganda kwa damu baada ya kupatwa na majeraha, ajali au mchubuko.

Huhusika pia katika kuimarisha mifupa.

3. Presha

Madini ya potassium yanayopatikana kwenye karoti huusaidia mwili katika kudhibiti ongezeko la msukumo wa damu unaoweza kusababisha shinikizo kubwa la damu.

Ni muhimu pia kwa watu wenye shinikizo kubwa la damu kwa kuwa hutoa mchango mkubwa katika kuepusha lisiongezeke zaidi.

Shinikizo kubwa la damu linaweza kuleta athari kwenye moyo pamoja na kusababisha kiharusi.

4. Saratani

Kwa mujibu wa National Cancer Institute, mwili wa binadamu hupokea kemikali na sumu nyingi zinazoweza kusababisha aina mbalimbali za saratani.

Uwepo wa lutein, beta carotena na zeaxanthin kwenye karoti huusaidia mwili katika kupambana na saratani, pamoja na kutoa kinga ili saratani husika zisitokee.

Tafiti kadhaa za afya zinasisitiza kuwa karoti inaweza kusaidia katika kupambana na saratani ya tezi dume, damu pamoja na mapafu.

5. Kisukari

Karoti ni miongoni mwa vyakula vyenye kiwango kidogo cha sukari.

Kwa kuwa watu wenye kisukari hushauriwa kutokutumia vyakula vyenye uwezo wa kutengeneza sukari nyingi, karoti inaweza kuwa chaguo sahihi kwao.

Sababu nyingine inayofanya karoti iwe chaguo zuri kwa watu wenye kisukari ni uwepo wa kiasi kikubwa cha nyuzi lishe.

Hii inatoa ishara kuwa haiwezi kuufanya mwili utengeneze na kutunza sukari nyingi hivyo ni salama kwao.

6. Kinga

Vitamini C haiishii kwenye maembe, limao na machungwa pekee.

Huwepo pia kwenye karoti.

Ni muhimu katika kujenga kinga imara ya mwili, kuwahisha uponaji wa vidonda pamoja na kuhakikisha kuwa mwili unakuwa na afya nzuri.

7. Sumu

Katika harakati za maisha ya kila siku, binadamu hutumia sumu kutoka kwenye vyakula, vinywaji pamoja na hewa kwa kujua au kutokujua.

Sumu hizi siyo rafiki kwa mwili.

Karoti huwa na viondoa sumu vingi ambavyo huusaidia mwili katika kuviondoa hivyo kuepusha athari mbaya zinazoweza kutokea kwa afya hasa kupunguza uwezekano wa kuugua magonjwa sugu.

Baadhi ya magonjwa hayo ni kisukari, shinikizo la juu la damu pamoja ma magonjwa ya moyo.

8. Moyo

Ushauri wa maana unaolenga kutunza afya ya moyo husisitiza kuongeza matumizi ya vyakula vyenye madini ya potassium na kupunguza vyakula vyenye sodium.

Karoti ni chakula kilicho na madini ya kutosha ya potassium.

Aidha, tafiti kadhaa zinabainisha kuwa vyakula vyenye potassium nyingi huukinga mwili usipatwe na ugonjwa wa kiharusi.

Tumia karoti ili ulinde moyo wako.

9. Choo Kigumu

Unasumbuliwa na tatizo la choo kigumu?

Tafuna karoti, au itumie kama kiungo kwenye chakula chako.

Nyuzilishe husaidia kulainisha choo.

Zipo za kutosha kwenye karoti.

10. Mifupa

Tafiti nyingi zinathibitisha kuwa vitamini K, calcium na phosphorus huboresha afya ya mifupa.

Aidha, huhitajika kwenye kuongeza ujazo wa mifupa na kuzuia tatizo la kuvunjika na kusagika kwake.

Karoti ni mzizi wenye uhakika wa kukupatia virutubisho vyote hivi kwa pamoja pasipo nyongeza ya kuhitaji virutubisho vingine.

Matumizi

Inaweza kutumika kwa kuitafuna, juisi pia kwa kuipika kama sehemu ya viungo vya chakula.

Kwa watu wanaotumia kama juisi, ni muhimu kutoisaga sana ili kutunza ubora na wingi wa virutubisho vyake.

Vivyo hivyo kwa watu wanao ipika.

Moto mkubwa usitumike, pia isipikwe kwa muda mrefu ili kuepuka changamoto ya kuharibu ubora wa virutubisho vyake.

Tahadhari

Ulaji wa karoti nyingi unaweza kubadilisha rangi ya ngozi kwa kuifanya iwe na rangi ya machungwa – manjano.

Huchangiwa na uwepo wa kiasi kikubwa cha beta carotene. Hii ni changamoto inayotibika yenyewe baada ya kupunguza matumizi yake.

Zinaweza pia kumfanya mhusika ajisaidie choo chenye rangi ya manjano. Hali hii haina athari kwa afya, huisha yenyewe baada ya kuacha au kupunguza matumizi ya karoti.

Pia, baadhi ya watu huwa na mzio wa karoti ambao midomo yao huwasha au kuvimba baada ya kuzitumia. Watu hawa wanashauriwa kutokutumia mzizi huu hadi pale ambapo changamoto hii itatatuliwa.

Share This Article