Ni upasuaji mdogo unaofanyika ili kuondoa ngozi ya mbele inayofunika sehemu za siri za mwanamme.
Asili ya utamaduni huu ni imani za kidini, ambazo baadae zilithibitishwa kuwa na faida kiafya. Leo, watu hutahiri kwa sababu za kiafya, au za kidini.
Mwanamme huzaliwa na ngozi inayofunika kichwa cha sehemu zake sa siri.
Kupitia tohara, ngozi hii huondolewa kwa kufanya upasuaji mdogo usiotumia muda mrefu sana, kati ya dakika 15-30.
Kwa sababu za kiusalama, pamoja na kuhakikisha kuwa tendo hili linafanyika kwa ufanisi mkubwa, ni vizuri kama likifanywa hospitalini.
Watoto wadogo wanaofanyiwa tohara huwa na faida kubwa ya kutokupata maumivu makubwa kama watu wazima, kutumia muda mchache zaidi kwenye upasuaji pia uponaji wa kidonda huchukua muda mfupi sana kati ya siku 7-10 pekee.
Imani Potofu
Tofauti na jinsi ambavyo watu wengi huamini, tohara haiwezi kudumaza afya ya sehemu za siri za mwanamme.
Ukuaji wa viungo vyote vinavyounda mwili wa binadamu huongozwa na mifumo rasmi iliyoshikizwa kwenye vinasaba vya urithi pamoja na homoni mbalimbali.
Msingi wa taarifa hizi hauwezi kuathiriwa kwa kukata ngozi ya mbele inayofunika sehemu hizo.
Kama ambavyo mtu huzaliwa akiwa na asili ya urefu, ufupi, macho makubwa au kipara na asiwe na uwezo wa kuibadili asili hii, vivyo hivyo kwa ukubwa au udogo wa maungo haya muhimu kabisa kwa afya ya uzazi wa mwanamme.
Tohara haiwezi kwa namna yoyote ile kuathiri ukuaji wa sehemu za siri za mwanamme pamoja na kupunguza msisimko wa tendo la ndoa kwa sababu kinacho ondolewa ni ngozi tu, siyo kichwa wala nyama ya sehemu hizo. (1)
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, miongozo ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) pamoja na kituo cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC), tohara huwa na faida nyingi kwa afya ya mwanamme mwenyewe, pamoja na mwanamke ambaye atashiriki naye tendo la ndoa.
Tohara hupunguza nafasi ya kupata maambukizi ya mara kwa mara kwenye mfumo wa mkojo hasa kwa watoto wadogo. (2,3)
Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa tohara sio kinga ya magonjwa ya zinaa. Saratani ya uume ni tatizo lisiloonekana sana, lakini hutokea kwa baadhi ya wanaume.
Tohara husaidia kutoa kinga dhidi ya tatizo hili.
Faida Zake
Kupitia tendo la ndoa, wanawake hunufaika pia na tohara ya wanaume kwa kuwapunguzia uwezekano wa kuugua saratani ya mlango wa kizazi.
Hii inatokana na ukweli kuwa wanaume walio tahiriwa huwa na uwezekano mdogo zaidi wa kubeba virusi aina ya Human Papillomavirus (HPV) ambavyo huhusishwa kwa kiasi kikubwa na saratani hii kuliko wanaume wasio tahiriwa. (4,5)
Tohara husaidia pia kurahisisha swala la usafi kwa mwanamme.
Ngozi hii huhifadhi uchafu wa aina nyingi, virusi pamoja na bakteria wabaya wanaoweza kuwa hatari kwa afya. Ngozi inapoondolewa, kazi ya mwanamme katika kuhakikisha usafi wa eneo hili huwa rahisi sana. (8)
Muda Sahihi
Tohara inaweza kufanyika muda wowote, kwa watoto wachanga pamoja na watu wazima.
Hata hivyo, watoto njiti, watoto waliozaliwa kwenye familia zilizo na historia ya uwepo wa matatizo katika mfumo wa damu (kuganda kwa damu) pamoja na wale walio zaliwa wakiwa na changamoto kadhaa kwenye afya zao hupaswa kusubiri kwanza hadi changamoto hizi zipatiwe ufumbuzi kwanza.
Katika dini za Kiyahudi, tendo hili la kiimani hufanyika siku ya 8 tangu kuzaliwa kwa mtoto. Kwa ujumla wake, jamii mbalimbali huamua kwa kadri wao wanavyoona inafaa ni lini hasa tohara ifanyike kwa vinaja wao wa kiume.
Tohara ni salama. Haipunguzi ukubwa wa sehemu za siri, haiondoi nguvu za kiume pia haina athari zozote kwa afya ya mwanamme.