Utapiamlo ni hali ya mtu pasipo kujali umri wake kuwa na upungufu, wingi kuzidi kiasi au pia kutokuwa na uwiano sawa wa nishati pamoja na virutubisho mwilini mwake.
Takwimu
Takwimu za shirika la Afya Ulimwenguni zinaonesha kuwa mwaka 2020 pekee, watoto milioni 149 duniani walio na umri chini ya miaka 5 wakiwa na ukuaji hafifu huku milioni 38.9 wakiwa na unene uliopita kiasi. (1,2)
Kila mwaka, asilimia 45 ya vifo vyote vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 vinavyotokea duniani huhusishwa na lishe duni.
Changamoto hii huonekana zaidi kwenye nchi masikini duniani, pamoja na zile zenye uchumi wa kati. (3,4)
Chakula ndio msingi mkuu wa afya bora. Kwa kutambua umuhimu huu, wataalam wa vyakula na lishe wameweka mgawanyo wa makundi matano ya vyakula, ambayo ni pamoja na
- Vyakula vya asili ya nafaka, mizizi, ndizi mbichi.
- Vyakula asili ya wanyama na jamii ya mikunde.
- Mbogamboga
- Matunda
- Sukari, mafuta na asali.
Ili mtu awe na afya bora, anapaswa kuhakikisha kuwa mlo wake wa kila siku unajumuisha makundi haya tajwa.
Mwongozo
Mwongozo wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuhusu unyonyeshaji unaelekeza wanawake wanyonyeshe watoto wao kwa walau miaka 2, huku miezi 6 ya mwanzo ikihusisha maziwa pekee ya mama pasipo kuchanganya vyakula vingine, au hata maji ya ziada kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya maziwa ya mama ni maji. (5)
Muongozo huu umekuwa haufuatwi ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kukosekana kwa uelewa, kutunza urembo wa maungo hasa matiti kwa kigezo cha kuogopa kuyaharibu pamoja na kukosekana kwa muda wa kutosha kulea watoto kutokana na sababu zinazotajwa kuwa za kujikwamua kiuchumi.
Matokeo yake, watoto wengi wamekuwa hawanyonyeshwi ipasavyo, na wengine wengi wamekuwa wahanga wa kuanzishiwa vyakula mbadala mapema, kabla hata hawajafikisha umri wa miezi 6.
Athari za mambo haya zimeanza kuonekana sasa. Watoto wengi wamekuwa wakisumbuliwa na upungufu mkubwa wa virutubisho vya protini, vitamini na madini.
Mfano halisi ni uwepo wa malalamiko mengi ya wazazi juu ya kutokuongezeka uzito pamoja na ukuaji hafifu wa watoto wao usio endana na umri.
Pamoja na uwepo wa sababu zingine, changamoto hii huhusishwa pia na upungufu wa protini ambayo ndio huhusika moja kwa moja kwenye ukuaji, kurekebisha seli, misuli na tishu za mwili zilizo umia pamoja na kuratibu kazi za mifumo mbalimbali ya mwili.
Protini inapokuwa chache hasa kwa mtoto mdogo, ni lazima ukuaji wake uwe mashakaki.
Uji wa Watoto
Wazazi na walezi wengi wamekuwa wanategemea matumizi ya uji wa lishe unaotengenezwa kwa nafaka ili kukudhi haja ya watoto wao. Lakini, ni ukweli kuwa waandaaji wengi wa unga huu, japo siyo wote, hutumia aina moja tu ya kundi la vyakula katika kuuandaa.
Wengi hutumia nafaka. Unga huo unaweza kuwa mchanganyiko wa ulezi, mahindi, mtama, uwele pamoja na mhogo. Huu ni mfano tu.
Bila shaka, unga huu hauwezi kutosheleza kukidhi mahitaji ya mtoto anayekua kwa kasi wakati huu.
Bahati mbaya zaidi, aina hii ya mlo imekuwa ikitegemewa kwa asilimia 100 katika makuzi ya mtoto. Asubuhi atapewa, mchana, hali kadhalika usiku.
Ni ungalishe kutwa mara tatu au nne. Watoto nao ni binadamu kama sisi, fikiria kama wewe ndiye ungepewa aina moja ya mlo kila siku. Usingekinai?
Lengo sio kubeza aina hii ya mlo, bali ni kuwashauri wazazi wa watoto kuwabadilishia chakula watoto wao.
Watoto wanapaswa kupatiwa makundi yote ya vyakula yaliyotajwa hapa.
Muhimu
Jambo la muhimu kukumbuka ni kuwa lazima chakula hiki kiwe laini sana, pia apatiwe matunda kwa mfumo wa juisi.
Kwa watoto walio na meno tayari, wenye uwezo wa kutafuna, wanaweza kupatiwa kipande kidogo cha tunda ili watafune wao. Faida zake ni nyingi zaidi kuliko juisi. (6,7)
Kwa wazazi, hakuna sheria inayotoa hukumu kwa watoto kuwa kila siku lazima wapatiwe mlo huu. Watoto wanahitaji kukua kimwili na kiakili, pia wanahitahi kujenga mfumo imara wa kingamwili zao. (8)
Watoto wabadilishiwe chakula, hawana shida kubwa ya nafaka kama ambavyo wanahitaji vitamini, protini na madini.
Haya yanapatikana kupitia vyakula vyenye asili ya wanyama, jamii ya mikunde, mbogamboga, matunda, sukari, mafuta na asali.