Wachumba: Vipimo 5 Muhimu kabla ya Ndoa

6 Min Read

Ndoa nyingi zimekuwa zinapitia changamoto kubwa ya migogoro na kutokuelewana kutokana na uwepo wa mapungufu fulani kwenye afya ya wanandoa husika.

Changamoto hizi mara nyingi huonekana baada ya kuanza kuishi pamoja, huwa pia hazijawahi kuzungumziwa au kuwekwa wazi kabla.

Kutokana na umuhimu wa jambo hili ambalo ndiyo kiini cha jamii, taifa na dunia nzima kwa ujumla, tumekuletea orodha ya vipimo maalumu vinavyoweza kufanywa na wachumba kabla ya kuelekea hatua ya mwisho ya kutangaza ndoa.

Vipimo hivi ni muhimu sana katika kutoa picha na muongozo wa mambo yatakayo tokea mbele ya safari hii ya kudumu, tumevieleza hapa chini kwa upana wake.

1. Damu

Muundo wa makundi ya damu hufanyiwa mgawanyiko kwa kutumia utaratibu wa ABO ambao hubeba tafsiri ya makundi yote ya damu duniani.

Sio kila mtu anaweza kumchangia damu mwenzie, pia baadhi ya makundi ya damu yakiingiliana wakati wa kutunga ujauzito yanaweza kuathiri afya ya mama na mtoto.

Mfano, mama mwenye kundi lolote hasi la damu akikutana na mwanamme mwenye kundi lolote chanya la damu huleta changamoto kwenye ujauzito hasa ule wa pili na kuendelea.

Mama anaweza kupata changamoto nyingi na watoto wanaweza kuwa wanafia tumboni kila mara.

Namna pekee ya kuepuka changamoto hii ni mwanamke huyu kupata sindano inayozuia athari za muingiliano huu wa damu wakati wa ujauzito, au ndani ya saa 72 baada ya kujifungua.

Pasipo kujua makundi ya damu kabla, wanandoa hawa watajipangaje kuzuia athari hizi? Mwisho wa siku wanaweza kujiingiza kwenye mambo yanayoamini katika ushirikina pasipo kufahamu kuwa hili jambo ni la kisayansi na huepukika kabisa.

2. Uzazi

Lengo mama la ndoa yoyote ni kuendeleza jukumu la uumbaji duniani.

Kila mtu huwa na ndoto hii kubwa ya kuzaa watoto.

Kuna vipimo kadhaa vinavyo mhusu mwanamke moja kwa moja na vingine huwahusu wanaume kama homoni, uhai wa mirija ya uzazi, uvimbe kwenye kizazi, uchunguzi wa mbegu za kiume n.k

Vipimo hivi huonesha uimara wa afya ya uzazi na kutoa uhakika wa baadae kama wachumba hawa wanaweza kupata watoto au la.

Badala ya kuishi kwa wasiwasi kama watoto watapatikana au la, ni muhimu sana kufanya vipimo hivi.

3. VVU na Magonjwa ya Zinaa

Wanandoa huletwa pamoja kupitia mambo mengi, lakini kihisia huunganishwa na tendo la ndoa ambalo hubeba dhima nzima ya uwepo wa ndoa.

VVU na magonjwa mengine ya zinaa mfano kisonono, kaswende, klamidia na masundosundo husambaa kwa kasi kubwa kupitia ushiriki wa tendo la ndoa (ngono).

Kwa kuwa tendo hili haliepukiki kwa wanandoa, ni muhimu kwao kupima kwanza magonjwa ili kujiandaa kisaikolojia kama wataamua kuendelea pamoja na kuepusha hatari ya kuambukizana na kupoteza uhai kwani baadhi yake huua.

Itasaidia pia kuchukua tahadhari muhimu katika kujikinga.

4. Magonjwa ya Kijenetiki

Taarifa za baadhi ya magonjwa hubebwa kwenye viini vya taarifa za urithi zilizo shikizwa ndani ya vinasaba (DNA) hivyo hurithishwa moja kwa moja kwa watoto kupitia wazazi wao.

Mfano wa magonjwa haya ni seli mundu, baadhi ya magonjwa ya moyo, saratani, misuli kukosa uwezo wa kufanya kazi pamoja na tatizo la kuganda kwa damu linalofahamika kama hemofilia.

Kupitia vipimo, wachumba wanaweza kutambua uwepo wa changamoto hizi hivyo kuwafanya wajiandae vizuri kuzikabili hapo baadae wakiwa kwenye ndoa.

5. Afya ya Akili

Unyanyasaji, kuuana, kushambuliana pamoja na kutelekeza watoto na familia ni mojawapo ya matatizo makubwa yanayoikumba jamii kwa sasa. Pamoja na sababu zingine, afya ya akili inaweza kuwa ni chanzo cha yote.

Kabla ya ndoa, jiridhishe kama mwezi wako sio chizi.

Hauwezi kumtambua kwa kumtazama pekee, pia siku za mwanzo za mapenzi hutawaliwa na maigizo mengi yanayoweza kunyima kuonekana kwa uhalisia wa tabia anuai za mtu.

Fikeni kwa wataalam wa afya ya akili mchunguzwe kwanza. Jamii imechoka kuzika watu kila siku.

Tafsiri Yake

Miaka ya hivi karibuni, elimu kubwa inayosisitiza umuhimu wachumba kupata vipimo hivi kabla ya ndoa imekuwa inatolewa.

Jambo hili halifanyiki kwa bahati mbaya, ni mkakati maalumu uliobeba malengo makuu 5 ambayo ni:

  • Kudhibiti ongezeko la magonjwa ya kurithi.
  • Kukazia umuhimu wa ndoa iliyojengwa kwenye msingi wa afya salama.
  • Kupunguza mzigo wa benki za damu pamoja na vituo vya afya kwenye kuhudumia wagonjwa wenye changamoto hizi.
  • Kuondoa changamoto za kisaikolojia na msongo mkubwa wa mawazo ambao familia nyingi hupitia baada ya kuathirika na mojawapo ya matatizo ambayo yangeepukwa kama vipimo vya awali vingefanyika kabla ya ndoa.
  • Kupunguza mzigo wa kiuchumi kwa familia na jamii nzima katika kuhudumia wagonjwa na wahanga wa mojawapo ya changamoto hizi.

Ndoa salama yenye mafaniko, furaha na amani hujengwa kwenye misingi ya afya bora.

Ni muhimu kwa kila anayepanga kufunga ndoa apate vipimo hivi kabla.

Share This Article