Miaka ya hivi karibuni, mijadala inayohusu afya ya uzazi wa mwanamme imeongezeka sana.
Wingi wa mijadala hii imejikita kwenye changamoto ya upungufu wa nguvu za kiume pasipo kufahamu kuwa afya ya uzazi wa mwanamme inahusisha mambo mengi kuanzia hisia, uzalishwaji na ubora wa mbegu za kiume, uwezo wa kushiriki tendo la ndoa, nafasi ya kurutubisha yai la mwanamke pamoja na afya ya tezi dume.
Kwa mujibu wa tafiti, tatizo la upungufu wa nguvu za kiume huathiri takriban moja ya tatu ya idadi ya wanaume wote duniani.
Kwa namna ya kipekee kabisa, leo tutajadili mbinu na aina mbalimbali za vyakula vinavyoweza kuboresha afya ya uzazi wa mwanamme kwa ujumla wake.
1. Spinach
Huwa na kiasi kikubwa cha madini ya folate ambayo huongeza mzunguko wa damu mwilini.
Tafiti kadhaa zinataja upungufu wa madini haya kuwa miongoni mwa sababu kuu za tatizo la upungufu wa nguvu za kiume. Fungu moja dogo la mboga hii lenye wastani wa 185 g hubeba zaidi ya 77% ya mahitaji ya folate kwa siku. (1,2,3)
Huwa pia na magnesium, madini yanayoboresha mzunguko wa damu mwilini pamoja na kuchochea uzalishwaji wa homoni za kiume.
2. Tikiti Maji
Ni tunda ambalo huwa na amino acids-citrulline ambazo hubadilishwa kuwa arginine kisha nitric oxide.
Hii hufanya kazi ya kupanua mishipa ya damu na kuongeza msukumo wake kwenye sehemu za siri za mwanamme.
Huitwa viagra ya asili. (4,5,6)
Kwa miaka mingi, tunda hili limekuwa linatumika katika kutatua changamoto mbalimbali za afya ya uzazi wa wanaume, hasa kuongeza uwezo wa kushiriki tendo la ndoa.
3. Karoti
Kwa wanaume wanaotaka kuongeza ubora wa mbegu zao wanapaswa kutumia karoti kwa wingi.
Karoti huwa pia na uwezo wa kuongeza uwezo mbegu za kiume kwenye kuogelea kutokana na uwepo mwingi wa carotenoids. (7,8)
Hizi ndio kemikali zinazoupatia mzizi huu rangi yake.
4. Nyanya
Uwepo mwingi wa virutubisho pamoja na viondoa sumu hutoa faida kubwa kwa afya ya uzazi wa mwanamme kwa ujumla wake.
Hulinda na kuimarisha uwezo wa mwanamme katika kumpa mwanamke ujauzito pamoja na afya ya tezi dume.
Lycopene na vitamini C zinazopatikana kwenye nyanya huhusishwa na ubora wa mbegu za kiume na kupunguza uwezekano wa kuugua saratani ya tezi dume. (9)
5. Vyakula Jamii ya Karanga
Huongeza uzalishwaji wa mbegu za kiume zilizo bora pamoja na kulinda vina saba (DNA) vya mbegu hizo.
Vyakula hivi huwa na kiasi cha kutosha cha asidi ya Omega-3, vitamini E, zinc pamoja na selenium.
Virutubisho hivi ni rafiki sana kwa afya ya mwanamme katika kuweka uwiano sawa wa homoni hivyo kutengeneza mazingira wezeshi ya utengenezwaji wa mbegu bora, zenye maumbo imara na nguvu kubwa ya kurutubisha yai ili ujauzito uweze kutungwa. (10,11)
Tumia karanga, almonds na korosho mara kwa mara, zitakusaidia.
6. Asali
Jamii ya kale ya Persia ilikuwa na utaratibu wa kuwafanya wanandoa wapya watumie asali mbichi kila siku kwa mwezi mzima kama njia ya kuongeza hamu na matamanio ya kushiriki tendo la ndoa.
Mwezi huu ulifahamika kama honey month au honeymoon.
Asali huwa na utajiri aina nyingi za vitamini B zinazohitajika kwenye uzalishwaji wa homoni za kiume.
Huwa pia na kiwango sahihi cha sukari za fructose ambazo huongeza stamina, kutoa uhakika wa nguvu za ushiriki wa tendo la ndoa pamoja na nguvu wezeshi kwa mbegu za kiume katika kuogelea na kupambana ndani ya mfereji wa uzazi wa mwanamke.
Asali yote inafaa pasipo kujali aina ya nyuki waliotumika kuitengeneza.
7. Vitunguu Saumu
Vitunguu saumu huongeza msukumo na usafirishwaji wa damu kwenye viungo vya uzazi wa mwanamme.
Hufanya hivyo kwa kuongeza wingi wa nitric oxide ambayo huifungua na kuipanua mishipa ya damu.
Tukumbuke kuwa pamoja na mambo mengine, msukumo wa damu wa kutosha ndio huamua uwezo wa mwanamme katika kuhimili tendo la ndoa.
Pamoja na kazi hiyo, kemikali zake za S-allyl cysteine huchochea uzalishwaji wa homoni za kiume.
Ni kiungo bora sana katika kuboresha afya ya uzazi wa mwanamme kwa ujumla wake.
8. Mazoezi
Ukiondoa mlo, ushiriki wa mazoezi yanayoongeza utimamu wa mwili hufaa sana katika kuongeza ubora wa afya ya uzazi.
Tafiti zinaeleza kuwa wanaume wanaofanya mazoezi huwa na vichocheo vingi vya kiume, pia mbegu zao huwa bora sana kuliko wale wasiofanya mazoezi. (12,13)
Hata hivyo, haushauriwi kufanya mazoezi magumu sana kwa muda mrefu kwani hayaweza kupunguza uzalishwaji wa vichocheo vya kiume.
Fanya kwa kiasi.
9. Tumia Maca
Utumiaji wa mzizi wa maca huongeza hamu ya kushiriki tendo la ndoa pamoja na kuongeza uwezo wa kushiriki tendo hili.
Asili ya mmea huu ni nchi ya Peru.
Mmea huu bado haujaonekana kuwa na faida kubwa katika kuongeza uzalishwaji wa vichocheo vya kiume. (14)
10. Tiba Lishe
Madini ya zinc husaidia kuongeza uzalishwaji wa vichocheo vya kiume pamoja na namba ya mbegu za kiume.
Vitamini D huhusishwa na kuongeza kasi ya uogeleaji wa mbegu za kiume. (14)
Vitamini C hufanya kazi nyingi ikiwemo kuongeza kinga ya mwili pamoja na kuharibu sumu zinazoshambulia seli za mwili. Baadhi ya tafiti zinathibitisha uwezo wa vitamini hii katika kuongeza uzalishwaji wa mbegu za kiume, kuongeza kasi ya kuogelea pamoja na kulinda maumbo yake yasiharibike. (15)
Virutubisho hivi unaweza kuvipata kutoka kwenye vyakula, au unaweza kununua madukani vikiwa vimeandaliwa kwa mfumo wa vidonge.
11. Punguza Stress
Mtu anapokuwa na mkazo au stress, mwili wake huzalisha kiasi kikubwa sana cha vichocheo vya cortisol.
Vichocheo hivi hudumaza afya ya uzazi na inaweza kuwa chanzo cha ugumba kwa wanaume.
Vichocheo hivi huathiri pia uzalishwaji wa vichocheo vya kiume ambavyo ndiyo huongoza tabia zote za kiume.
Ni ngumu kuzuia hali hii lakini pambana uwezavyo uishinde.
12. Tumia Ashwagandha
Mmea huu umeanza kutumika tangu zamani sana nchini India miaka ya 6000 K.K kwenye kutibu changamoto mbalimbali za afya hasa stress, wasiwasi, kisukari, kuongeza kumbukumbu pamoja na kuboresha mfumo wa fahamu.
Huongeza uzalishwaji wa vichocheo vya kiume, idadi ya mbegu za kiume pamoja na kasi yake kwenye kuogelea. (16)
Unaweza kutafuta virutubisho hivi kwenye maduka ya dawa.
13. Tangawizi
Tangawizi huongeza uzalishwaji wa vichocheo vya kiume, hupunguza uharibifu wa kuta za ndani ya korodani, huondoa sumu pamoja kupanua mishipa ya damu inayoelekea kwenye uume.(17)
Ifahamike kuwa ufanisi wa tendo la ndoa kwa mwanamme pamoja na mambo mengine, hutegemea pia ukubwa wa msukumo wa damu kuelekea sehemu za siri.
Tangawizi hufanya kazi hii zote kwa ufanisi mkubwa sana.
Muhtasari
Asilimia 10 ya wanaume wote wanaojaribu kutafuta watoto nchini Marekani hukabiliwa na changamoto ya ugumba huku asilimia 40-50 ya visa vyote vya changamoto za kupata watoto kwenye mahusiano duniani vinasababishwa na wanaume.
Hii inamaanisha kuwa kutoa mbegu za kiume pekee hakuwezi kuthibitisha ubora wa afya ya uzazi.
Sababu za kuwahi kufika kileleni zinafahamika pamoja na mbinu za kuondoa tatizo hili zipo wazi pia.
Fuatilia mbinu hizi kwa pamoja ili uweze kuondoa changamoto zote zinazohusu afya yako.