Vitunguu Saumu: Virutubisho, Faida na Tahadhari kwa Afya

6 Min Read

Kisayansi huitwa Allium sativum, kinapatikana katika kundi dogo zaidi la familia ya Liliaceae.

Pamoja na uwepo wa viambatao vingine, kemikali kuu inayopatikana kwenye kitunguu saumu ni Alliin ambayo hubadilishwa kuwa Allicin kisha Diallyl sulphide.

Sifa kuu ya kemikali hizi ni kuwa zina sulphur ndani yake na ndiyo huvipa ladha na harufu yake.

Virutubisho

Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), vitunguu saumu huwa na maji, nishati, protini, nyuzi lishe, madini ya chuma, magnesium, phosphorous, potassium na sodium.

Aidha zinc, copper, vitamini C, niacin, folate pamoja na viondoa sumu huwepo kwenye kiungo hiki.

Vitunguu saumu huwa na faida zifuatazo kwa afya;

1. Presha

Magojwa ya mfumo wa damu na moyo huathiri namba kubwa ya watu duniani.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu bilioni 1.28 wanakabiliwa na changamoto hii duniani.

Uwepo wa shinikizo kubwa la damu ndio sababu kubwa iliyojificha nyuma ya magonjwa haya.

Tafiti mbalimbali zilizofanyika kwa binadamu zinaonesha kuwa kitunguu saumu kinaweza kupunguza shinikizo kubwa la damu. (1,2,3)

2. Mafuta

Huongeza kiasi cha mafuta yanayofaa mwilini na hupunguza mafuta yasiyofaa kwenye mzunguko na mishipa ya damu kwa ujumla wake. (4,5)

Hii ina faida kwa watu wenye uzito uliozidi, pia wale wanaosumbuliwa na shinikizo la juu la damu.

Jiepushe na changamoto hii kwa kutumia vitunguu saumu.

3. Vimelea

Mojawapo ya mafanikio makubwa ya kitunguu saumu ni uwezo wake wa kupambana na bakteria wa kifua kikuu, S. aureus wanaosababisha matatizo mbalimbali ya ngozi na mfumu wa upumuaji pamoja na S. faecalis wanaosababisha matatizo kwenye mfumo wa mkojo. (6,7,8)

Hii isitumike kama tiba mbadala katika matatizo haya, bali itumiwe pamoja na dawa za hospitalini ili kuimarisha zaidi afya ya mhusika.

4. Mafua

Vitunguu saumu huongeza uimara wa kinga ya mwili katika kupambana na magonjwa.

Utafiti mmoja uliohusisha matumizi ya vitunguu saumu kwa muda wa wiki 12 mfululizo ulionesha kupunguza changamoto ya mafua kwa asilimia 63.

Idadi ya siku za kuonesha dalili za ugonjwa huu zilipungua pia kwa asilimia 70 kutoa siku 5 hadi siku 1.5. (9,10,11)

Hata hivyo, tafiti zaidi zinahitajika katika kufafanua zaidi nadharia hii.

5. Mifupa

Hakuna utafiti wowote uliowahi kufanyika kwa binadamu ili kuthibitisha faida za kitunguu saumu kwenye afya mifupa.

Hata hivyo, tafiti nyingi zilizofanyika kwenye wanyama zinaonesha kuwa vitunguu saumu huwa na uwezo wa kuongeza uimara wa afya ya mifupa hasa kwa wanawake. (12,13,14)

Hufanya hivi kwa kuongeza kiwango cha vichocheo vya estrogen.

6. Uzazi

Kwa wanaume huongeza msukumo wa mzunguko wa damu kwenye sehemu za siri hivyo kuboresha ufanisi wa tendo la ndoa, pia huchochea uzalishwaji wa mbegu bora za kiume.

Kwa wanawake huwakinga dhidi ya changamoto mbalimbali za mfumo wao wa uzazi hasa zile zinazosababishwa na bakteria. (15,16)

Tumia vitunguu saumu kwa afya bora ya uzazi.

7. Saratani

Mei 2013, Jarida la Asian Pacific Journal of Cancer Prevention lilichapisha majibu ya utafiti uliofanyika kwa miaka mingi kuhusu uhusiano wa ulaji wa vitunguu saumu na uwepo wa saratani ya tezi dume.

Utafiti huu ulitoa hitimishisho linaodokeza juu ya uwezo wa vitunguu saumu katika kupunguza hatari ya kuugua tezi dume. (17)

Hata hivyo, tafiti zingine zinahitajika ili kufafanua zaidi hoja hii.

8. Kujifungua Kabla ya Wakati

Maambukizi ya vijidudu vya magonjwa wakati wa ujauzito huongeza nafasi ya mwanamke kujifungua kabla ya muda sahihi.

Katika utafiti uliofanywa na Norwegian Institute of Public Health, unaonesha kuwa wanawake wajawazito wanaotumia vitunguu saumu huwa na nafasi ndogo ya kupatwa na maambukizi ya mara kwa mara ya magonjwa, hasa yale yanayosababishwa na virusi na bakteria. (18)

Utafiti huu unasisitiza matumizi ya vitunguu saumu kwa wanawake wajawazito kwani havina athari zozote kwa afya yao.

9. Sumu

Kitunguu saumu huwa na kiasi kikubwa cha viondoa sumu.

Husaidia kulinda vinasaba pamoja na seli za mwili ambazo ni kitovu cha uhai, pia huukinga mwili usipatwe na magonjwa sugu yasiyo ambukizwa hasa kisukari na presha. (19,20,21)

Unasubiri nini kuanza kutumia kiungo hiki?

10. Moyo

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wastani wa watu milioni 19.7 hufariki kila mwaka duniani kutokana na magonjwa ya moyo.

Kwa kuwa vitunguu saumu huwa na uwezo wa kuharibu mafuta mabaya pamoja na kupunguza shinikizo la juu la damu, uwezo wake katika kuulinda moyo hauwezi kutiliwa shaka. (22,23)

Hufaa kwa kila mtu, siyo kwa wagonjwa wenye changamoto za moyo pekee

11. Sukari

Tafiti kadhaa za afya zinabainisha uwezo wa vitunguu saumu katika kudhibiti ongezeko la sukari mwilini, pamoja na kuleta ahueni kwa wagonjwa, hasa wale wenye aina ya pili ya kisukari.

Huwa na kiasi kidogo cha nishati, pia huongeza uwezo wa vichocheo vya insulin katika kudhibiti sukari. (24)

Ni mzizi usio na gharama kubwa kuupata, utumie sasa kujikinga na kisukari.

Tahadhari

Matumizi makubwa ya vitunguu saumu hasa kwenye tumbo lisilo na chakula yanaweza kusababisha kujaa kwa gesi, mvurugiko wa tumbo pamoja na kuharibika kwa uwiano wa bakteria wazuri wanaolinda mfumo wa chakula. (25)

Vitunguu saumu vitumike baada ya kutumia vyakula vingine, au viongezwe moja kwa moja kwenye mapishi kama sehemu ya viungo ili kuepusha adha hii.

Share This Article