Upande Sahihi wa Kulala Wakati wa Ujauzito

2 Min Read

Wanawake wajawazito hushauriwa walalie upande wa kushoto au kulia.

Ushauri huu hulenga kuondoa athari pamoja na kuboresha afya ya mama na mtoto aliyeko tumboni.

Katika kuzingatia mazingira ya mfumo wa uzazi wa mwanamke hasa kwenye nyumba ya uzazi ambapo ndipo mtoto huyu hutunzwa, kulalia upande wa kushoto huwa ni bora zaidi kuliko upande wa kulia.

Husaidia usafirishwaji wa hewa ya kutosha na virutubisho vingi kwenda kwa mtoto kupitia kondo la uzazi.

Mapendekezo haya yanaweza yasikupe uhuru mkubwa sana kwa kuwa hukuzoea kabla kulala upande upande, lakini kwa wakati huu ni muhimu sana kuzingatia maana utajitengenezea mazingira mazuri ya wewe kuwa salama nyakati zote.

Kulalia Mgongo

Husababisha maumivu makali ya mgongo, kugandamiza mishipa muhimu ya fahamu, bawasiri, presha ya kushuka, choo kigumu, kukata kwa pumzi pamoja na kupungua kwa usambazwaji wa hewa na virutubisho kwenda kwa mtoto.

Sababu ya matatizo haya yote ni moja tu, mgandamizo mkubwa hutokea kwenye utumbo na mishipa mikubwa ya damu hasa ile ya Aorta na Vena cava.

Kulalia Tumbo

Inaweza pia kutegengeza mgandamizo mkubwa kwa mtoto lakini pia mwanamke mwenyewe hatakuwa na uhuru katika kusinzia.

Muhtasari

Kwa muktadha huu, ni muhimu sana kwa mwanamke mjamzito kulalia upande wa kushoto mara kwa mara bila kujali umri wa ujauzito.

Pale anapokuwa anajihisi kuchoka au maumivu, anaweza kulalia pia upande wa kulia kwa muda.

Pamoja na ukweli kuwa mtindo huu wa kulala hufaa ufuatwe kwenye kipindi chote cha ujauzito, miezi 3 ya mwisho ndiyo hubeba umuhimu mkubwa zaidi.

Ni wito wetu kwa wanawake wajawazito kufuata ushauri huu muhimu katika kupunguza changamoto mbalimbali za uzazi zinazoweza kuepukika.

Share This Article