Mdalasini: Aina, Virutubisho na Faida kwa Afya

7 Min Read

Ukiondoa kazi yake ya kuongeza ladha ya chakula, mdalasini hukusaidia pia katika mambo kadhaa ambayo hukuwahi kuyajua.

Kama zilivyo dawa au virutubisho vingine vya asili, mdalasini hufanya pia kazi hizi taratibu lakini kwa ufanisi mkubwa.

Virutubisho 

Pengine hukuwahi kudhani kama mdalasini huwa na mjumuiko wa aina mbalimbali za virutubisho.

Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), mdalasini huwa na mafuta, protini, wanga, nyuzi lishe, calcium, potassium, beta carotene pamoja na vitamini A. Aidha, huwa pia na kiwango kidogo cha sukari, madini ya chuma, selenium na vitamini C.

Pia, huwa na kemikali za cinnamaldehyde ambazo ndio huupa ladha na harufu yake. Cinnamate, cinnamic acid na aina mbalimbali za mafuta halisi ni miongoni mwa viambato vyake.

Aina za Mdalasini

Kuna aina kuu nne za mdalasini, lakini watafiti hupenda hutumia aina mbili za mdalasini ambazo ni Cinnamon cassia pamoja na mdalasini halisi, Cinnamomum verum.

Katika tafiti nyingi, kazi za mdalasini husomwa bila kujali sana aina ya mdalasini uliotumika kwa maana aina zote hizi hutofautiana kidogo sana kwa viwango vya kemikali zake.

Mdalasini huwa na faida nyingi sana kwa afya ya binadamu.

Baadhi ya faida hizo zimeelezewa hapa chini;

1. Uvimbe

Kutokana na uwepo wa flavonoids pamoja na Quercetin, gnaphalim na hesperidin, mdalasini unaweza kuzuia, kukinga na ikiwezekana hata kuondoa aina mbalimbali za uvimbe mwilini kwa kuzuia uzalishwaji wa nitric oxide.

Nitric oxide ni mojawapo ya kemikali za mwili ambazo hufanya ushenga katika kuchochea kutokea kwa uvimbe mwilini. (1,2)

Ulinde mwili wako dhidi ya aina mbalimbali za uvimbe kwa kutumia mmea huu.

2. Vimelea 

Mdalasini huwa na faida ya kupambana na vimelea pamoja na vijidudu vya magonjwa hasa bakteria na virusi.

Mvuke wa mafuta ya mdalasini pamoja na karafuu ikitumika kwa pamoja huwa na faida ya kupambana na S. choleraesuis na E. coli ambao husababisha matatizo ya mfumo wa chakula na ugonjwa wa UTI. (3,4,5)

Aina zingine pia za maambukizi  hasa zile za fangasi wa ulimi, uke na kibofu cha mkojo huweza kupunguzwa, au hata kuondolewa kabisa na mdalasini.

3. Chunusi

Ili mdalasini ukuondolee chunusi inabidi unga wake uchanganywe na asali.

Kama ilivyo kwa mdalasini, asali pia huwa na tabia ya kupambana na bakteria.

Kutumia viambato hivi kwa wakati mmoja kutakupa faida kubwa zaidi, bakteria wote wanaosababisha kutokea kwa chunusi wataondolewa. (6)

Unatakiwa kuchukua unga kiasi wa mdalasini kisha changanya na kiasi kidogo cha asali ili utengeneze mchanganyiko mzuri.

Tumia mchanganyiko huo kupaka usoni mwako au kwenye sehemu iliyo na chunusi kisha safisha baada ya dakika 15, unapaswa kufanya hivi mara mbili kwa siku.

4. Sukari

Majaribio kwenye wanyama yanaonesha kuwa mdalasini unaweza kushusha sukari mwilini.

Jambo hili huenda sambamba na kupungua kwa lehemu mbaya hivyo kuboresha afya ya moyo kwa wagonjwa wa kisukari.

5. Mfumo wa Chakula

Mafuta ya cinnamaldehyde husaidia kuboresha mfumo wa chakula.

Hutengeneza mazingira rafiki kwa ukuaji wa bakteria wazuri wanaopatikana tumboni pamoja na kusaidia kupunguza gesi.

Ni kiungo muhimu sana kisichopaswa kukosekana jikoni kwako.

6. Polycystic Ovary Syndrome (PCOS)

PCOS ni tatizo linalowapata wanawake ambalo huvifanya vifuko vya mayai ya uzazi vitengeneze uvimbe mdogo mdogo kwenye kuta zake za nje.

Kwa mujibu wa PCOS Awareness Association, matumizi ya mchanganyiko wa unga au maji ya mdalasini pamoja na asali mbichi husaidia sana katika kupambana na changamoto hii. (7)

Kwa mujibu wa tafiti, takriban asilimia 4-20 ya wanawake wanakabiliwa na changamoto hii.

7. Sumu

Unapokuwa unazungumzia viungo vyenye kiasi kikubwa cha viondoa sumu hauwezi kuacha kuutaja mdalasini.

Huukinga mwili usipatwe na magonjwa sugu pamoja na kuzilinda seli za mwili wako ambazo ndiyo kiini uhai.

Athari zingine za sumu hizi ni kusababisha uzee wa haraka na magonjwa ya akili.

8. Saratani

Tafiti zinabainisha kuwa kemikali asilia za cinnamic aldehyde hudhibiti ukuaji wa seli zinazoweza kusababisha saratani ya mapafu maarufu zaidi kama A549 pamoja na seli za saratani za matiti (MCF-7).

Mdalasini unaweza pia kupambana, pamoja na kuzifanya zijiue zenyewe seli zinazosababisha saratani ya tezi dume kwa kuingilia mfumo wa taarifa zake. (8,9)

Matumizi ya mara kwa mara ya mdalasini yataupa mwili kinga ya kutosha katika kupambana na saratani mbalimbali mwilini, mfano ni zile zilizo tajwa hapa.

9. Moyo

Moyo ndiyo pampu inayosukuma damu mwilini, kuanzia siku ya 22 ya kutungwa kwa ujauzito hadi siku ya kufa.

Hufanya kazi hii kwa uamimifu mkubwa sana mchana na usiku, bila kuchoka.

Mdalasini huwa na tabia ya kuharibu mafuta mabaya yanayo jikusanya kwenye mishipa ya damu, hudhibiti shinikizo la damu, huimarisha mishipa ya damu pamoja na kuulinda moyo kwa ujumla wake.

Ni kiungo bora sana katika kuiongezea ufanisi pampu hii wako hasa kwa watu wenye magonjwa kama kisukari ambayo huhatarisha afya yake.

10. Ubongo

Umewahi kumuona mtu wa umri wa makamo ambaye mikono yake kila muda huwa inatetemeka?

Au hawezi kutembea vizuri kwa kuwa miguu yake, au mwili mzima kwa ujumla unatetemeka?

Huu ni mojawapo tu ya ugonjwa ambao asili yake ni uwepo wa udhaifu fulani kwenye ubongo.

Mdalasini hutajwa kuwa na uwezo wa kukinga ugonjwa huu, pamoja na kupunguza athari kwa wagonjwa.

Huitwa ugonjwa wa pankisoni.

11. VVU

Mdalasini unatazamiwa kutumika kwa siku za mbeleni kwenye kukabiliana na janga la ugonjwa wa UKIMWI.

Kwanini?

Hudhibiti HIV-1 isiingie kwenye seli za mwili ambayo baadae huanza kushambulia, kisha kusababisha upungufu wa kinga mwilini.

Aidha, tafiti kadhaa zimebaini kuwa mdalasini huamsha Tim-3 na PD-1 ambazo huongeza ufanisi wa chembe nyeupe za damu kwenye kupambana na HIV-1. (10,11)

Kampaundi za procyanidin ndizo huhusika kwenye kufanikisha kazi hii.

Muhtasari

Uwepo wa aina nyingi za mdalasini usikupe mashaka.

Mkusanyiko wa virutubisho na kemikali zake huwa hautofautiani sana.

Aidha, haupaswi kusitisha matumizi ya dawa rasmi za hospitalini kwa kuwa mdalasini kama ilivyo virutubisho vingine huleta majibu taratibu sana.

Share This Article