Wakati wa ujauzito, mwili huzalisha wastani unaokadiriwa kufikia hadi asilimia 50 ya damu na maji ya ziada ili kukidhi haja ya mtoto anayekua kwa kasi tumboni. (1)
Kuvimba kwa baadhi ya viungo vya mwili ni moja wapo ya matatizo makubwa ambayo huwakabili wanawake wajawazito wakati huu.
Uvimbe wa kawaida mara nyingi huonekana kwenye mikono, miguu, maungio ya mwili, nyayo za miguu na uso. (2)
Kuongezeka kwa maji wakati huu husaidia kuulainisha mwili ili uweze kutanuka na kuhimili ukuaji wa mtoto aliyeko tumboni.
Ongezeko hili la vimiminika huhitajika ili kuulaninisha mwili hivyo kuuruhusu utanuke kuendana sambamba na takwa la lazima la ukuaji wa mtoto.
Ifahamike kuwa umbo la mtoto huongezeka siku hadi siku hivyo ni lazima mwili wa mama utanuke pia kukidhi haja hii.
Mabadiliko haya huziandaa vizuri pia nyonga za mama ili ziweze kuwa na uwezo madhubuti wa kupanuka wakati wa uchungu wa kujifungua.
Ongezeko hili la vimiminika huchangia zaidi ya asilimia 25 ya uzito wote wa ziada wakati wa ujauzito.
Changamoto hii inaweza kuonekana wakati wowote wa ujauzito, lakini kwa wanawake wengi hudhihirika kiasi kikubwa kuanzia mwezi wa 5 wa ujauzito, na huendelea kuongezeka kadri ujauzito unavyozidi kuwa mkubwa zaidi.
Nini Kifanyike?
Kuna mambo kadhaa ambayo mwanamke mjamzito anaweza kufanya ili kuzuia kutokea kwa tatizo hili.
Mambo haya yanaweza pia kupunguza ukubwa wa tatizo kwa wanawake ambao tayari miili yao imeshavimba.
1. Chumvi
Chumvi ya mezani huwa na madini ya sodium ambayo huufanya mwili wa binadamu utunze maji ya ziada.
Mwanamke mjamzito anashauriwa kupunguza matumizi ya chumvi ambayo huulazimisha mwili uhifadhi kiasi kikubwa cha maji hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa uvimbe. (3,4,5)
2. Virutubisho
Mama mjamzito anashauriwa kutumia vyakula na virutubisho vyenye utajiri wa madini ya potasiam ili kuusaidia mwili katika kudhibiti ongezeko kubwa la maji. (6)
Baadhi ya vyakula hivyo ni viazi vitamu, ndizi, spinach, maharage, mtindi na samaki.
3. Mazoezi
Msaada mkubwa unaofaa katika kujikinga pamoja na kutibu tatizo hili ni kufanya mazoezi mepesi tu kila siku hasa yanayohusisha kutembea.
Mama mjamzito anapaswa kutenga muda kiasi wa kutembea kwa miguu pamoja na kufanya kazi ndogo ndogo za nyumbani zitakazokuruhusu awe anahama kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Kitu kikubwa kinachosababisha wanawake wengi wapatwe na hali hii ni kuendekeza sana kukaa, kuacha kufanya kazi na kulala sana kila muda kwa kudhani kuwa ni nzuri kwao. Hii sio kweli.
Ni muhimu kufanya mazoezi walau kidogo kila siku isipokuwa kwa wanawake waliozuiwa kufanya hivyo na daktari kwa ajili ya usalama wao pamoja na mtoto aliyeko tumboni. (7,8)
Dakika 30 kila siku kwa siku 5 za wiki ni kiwango cha kawaida ambacho hushauriwa.
4. Maji
Hii inashangaza kidogo. Inakuwaje mtu aliyevimba mwili ashauriwe kunywa maji mengi?
Mara nyingi, mwili unaopohisi kuwa unakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji hulazimisha mifumo yake inayohusika na udhibiti wa maji itunze kiasi fulani cha maji mwilini.
Unywaji wa maji mengi huzifanya figo ziongeze kasi ya utoaji wa maji ya ziada pamoja na taka mwili zingine. (9,10)
Kunywa maji ya kutosha.
5. Massage
Husaidia kuboresha usafirishwaji wa damu na vimiminika mwilini. (11,12)
Hufaa zaidi ikifanywa kwenye sehemu au viungo vya mwili vilivyo na uwezekano mkubwa zaidi wa kuvimba.
Mwanamme anaweza kuwa msaada mkubwa zaidi katika kukamilisha kazi hii.
6. Miguu
Wakati wa kukaa au kulala, mwanamke mjamzito anashauriwa kuweka miguu yake usawa wa juu kidogo kuzidi kifua chake.
Pia, hushauriwa uvaaji wa soksi maalumu za kubana.
Husaidia kurudisha maji na damu kutoka miguuni kuja sehemu ya juu ya mwili, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la kuvimba. (13,14)
Mwanzoni inaweza kuwa ngumu, jikaze utaweza.
Muhtasari
Kuvimba kwa mwili hasa miguu, mikono na maungio ni jambo la kawaida kabisa wakati wa ujauzito.
Ni uthibitisho wa wazi wa mapambano makubwa ambayo mwili hupitia ili kuuhifadhi uhai mpya.
Hata hivyo, katika nyakati chache, kuvimba kwa mwili kunaweza kuwa dalili mbaya ya uwepo wa changamoto kubwa za kiafya hasa kifafa cha mimba.
Husababisha ongezeko kubwa la shinikizo la damu wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua.
Maana nyingine ya kutokea kwa uvimbe ni uwepo wa damu iliyoganda kwenye mishipa ya damu maarufu zaidi kama deep vein thrombosis (DVT).
Tatizo hili huathiri mzunguko wa damu mwilini. (15,16)
Katika mazingira haya yote, unapaswa kuonana na daktari ikiwa;
- Uvimbe wa ghafla umetokea kwenye miguu, maungio, mikono au uso
- Kizunguzungu
- Macho kuona ukungu
- Maumivu makali ya kichwa
- Changamoto katika kupumua
- Kuweweseka
Pata msaada haraka.