Kitovu cha Mtoto Kujizungusha Shingoni Wakati wa Ujauzito

5 Min Read

Hali hii hufahamika zaidi kama Nuchal cord.

Ni kitendo cha kitovu cha mtoto kujizungusha kwenye shingo yake kwenye muda wowote ule wa ujauzito au wakati wa uchungu wa kuzaa.

Kitovu hubeba hewa, virutubisho, damu pamoja na kuruhusu ubadilishanaji wa taka mwili kati ya mama na mtoto.

Tatizo lolote linalohusisha kitovu linaweza kuwa hatari kwa afya ya mtoto kama halitashughulikiwa kwa wakati sahihi, kwa usahihi. (1,2)

Nafasi ya Kutokea 

Hali hii sio ya kushangaza sana.

Katika kila watoto 100 wanaozaliwa, walau watoto 25 kati yao huwa na changamoto hii.

Sababu

Wakati wa ujauzito, watoto huelea kwenye mfuko wenye maji ya uzazi.

Mfuko huu huwaruhusu watoto wazunguke, wacheze pamoja na kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine wakiwa ndani yake.

Japokuwa wanawake wajawazito husubiri kwa hamu matukio haya, pamoja na kufurahia pale yanapotokea, huwa na upande mwingine mbaya wa kusababisha kujizungusha shingoni kwa kitovu.

Sababu zingine za kutokea kwa hali hii ni

  • Kuwa na kitovu kirefu sana
  • Mfuko wa uzazi kuwa na maji mengi sana
  • Kuwa na ujauzito wa mtoto zaidi ya mmoja (3,4,5)

Dalili

Hakuna dalili za wazi za uwezo wa tatizo hili.

Hakuna mabadiliko yoyote ya kimwili anayoweza kuhisi mama mjamzito, au hata mabadiliko kwenye dalili za ujauzito.

Kwa ufupi, tatizo hili halina dalili yoyote.

Ugunduzi

Kipimo cha Ultrasound kinaweza kugundua uwepo wa changamoto hii.

Baada ya ugunduzi huu, mtaalamu wa afya atakueleza ukubwa wa tatizo hili na nini kifanyike ili kufanikisha zoezi la kuuleta salama uhai huu mpya duniani.

Bila kujali kuwa hali hii imegunduliwa kipindi cha awali kabisa cha ujauzito au muda mchache kabla ya kujifungua, mwanamke mjamzito anashauriwa kuchukulia hali hii kama jambo la kawaida.

Wataalamu wa afya watakushauri na kukuelekeza mambo kadhaa ya kufanya na kufuata wakati wote wa ujauzito pamoja na kipindi cha kujifungua ili kuzuia athari zozote mbaya zinazoweza kutokea kutokana na uwepo wa changamoto hii

Kinga

Hakuna kinga ya kuzuia au tiba ya kuondoa kutokea tatizo hili.

Ikitokea tatizo hili limegunduliwa kabla ya siku ya kujifungua, hakuna hatua yoyote ya ziada itakayochukuliwa isipokuwa kusubiria muda sahihi wa kujifungua ili msaada wa haraka uweze kutolewa katika kuhakikisha kuwa afya ya mtoto inabaki salama.

Athari

Katika mazingira ya kawaida, hali ya kitovu cha mtoto kujizungusha shingoni huwa haina athari yoyote kwa afya ya mama na mtoto mwenyewe.

Athari chache zinaweza kuonekana wakati wa kujifungua ikiwa kitovu hiki kitagandamizwa.

Wakati huu, upungufu mkubwa wa damu, hewa na virutubisho unaweza kutokea kwa mtoto. (6,7)

Ni nadra sana kutokea kwa changamoto kubwa kutokana na uwepo wa tatizo hili.

Baadhi ya changamoto hizo ni;

  • Kuongezeka kwa mapigo ya moyo ya mtoto
  • Kujifunga mafundo kwa kitovu
  • Kupungua kucheza kwa mtoto
  • Kupungua kwa kasi ya ukuaji wa mtoto
  • Kuongezeka kwa asidi kwenye damu
  • Kufariki akiwa tumboni

Mtoto anaweza kuzungukwa na kitovu chake mara nyingi na bado akawa na afya njema.

Inapotokea tatizo hili limegunduliwa mapema, au hata wakati uleule wa kujifungua mama mjamzito hapaswi kupata mshituko na wasiwasi kuhusu usalama na afya ya mtoto.

Kujifungua

Njia ya kujifungua kawaida ndio hufanyika kwa wanawake wengi.

Ifahamike kuwa, katika mazingira ya kawaida kitovu kujizungusha shingoni siyo jambo la dharura.

Inaweza kuchukuliwa kama dharura ikiwa tu itakuwa na madhara makubwa kwa mtoto kwa wakati huo

Nafasi ya kujifungua kwa upasuaji ni ndogo ikiwa hakuwa viashiria vyovyote vya hatari.

Muhtasari

Ni muhimu kukumbuka kuwa hali hii haiwezi kuzuiwa ili isitokee, wala hakuna kitu kibaya ambacho mama mjamzito hufanya ambacho hupelekea kutokea kwa hali hii.

Katika mazingira yote haya, mama mjamzito anashauriwa kuhudhuria kliniki yake mara kwa mara pamoja na kupanga ratiba zake vizuri ili awe tayari kujifungulia hospitalini pale muda sahihi utakapofika.

Uwepo wake kwenye kituo cha afya kutarahisisha utatuaji wa changamoto zote zinazoweza kutokea wakati wa kujifungua ambazo huhusiana na hali hii.

Share This Article