Hedhi ni utaratibu wa utokaji wa damu pamoja na uchafu mwingine kwenye sehemu za siri za mwanamke kila mwezi, ambao kwa lugha zingine zilizozoeleka sana mitaani huitwa period au kwenda mwezini.
Jambo hili la asili na kibaiolojia huchukua mzunguko wa siku kadhaa zinazokadiriwa kuwa kati ya 21–35.
Pamoja na uwepo wa aina nyingi ya mizunguko hii ya hedhi, mzunguko wa wastani wa siku 28 ndio maarufu zaidi na huonekana kwa wanawake wengi kuliko mizunguko mingine. (1,2)
Sababu
Wastani wa umri wa wasichana wengi kupata hedhi yao ya kwanza huwa ni kati ya miaka 8-15.
Hata hivyo, wakati wa ujauzito, kiasi kikubwa cha vichocheo vya progesterone na estrogen huzalishwa kwenye mwili wa mwanamke ambavyo huingia pia kwenye mwili wa mtoto kupitia kondo la uzazi.
Jambo hili halina maana mbaya, wala halina athari zozote kwa afya ya mtoto.
Baada ya kuzaliwa, watoto huvikosa vichocheo hivi ambavyo tayari miili yao ilikuwa imezoea kuishi navyo kupitia mama zao.
Kwa upekee kabisa, kupungua kwa ghafla kwa vichocheo hivi huwafanya watoto wenye jinsia ya kike waanze kutoa kwenye sehemu zao za siri uchafu wenye rangi ya maziwa au wakati mwingine damu.
Kitendo hiki cha kushangaza hufahamika zaidi kama hedhi feki au hedhi ya uongo. Hutokea kati ya siku ya 2-8 baada ya kuzaliwa kwa mtoto.
Ni Sawa?
Hedhi hii ya uongo hushitua wazazi wengi na huwafanya wapate changamoto kubwa katika kutafuta suluhisho lake.
Pamoja na kutisha kwake, haina madhara yoyote, pia haitoi maana yoyote mbaya kuhusu afya ya mtoto husika.
Ni hali ya kawaida kabisa ambayo hupona yenyewe tu ndani ya muda mfupi (wastani wa siku 2) tangu ionekane kwa mara ya kwanza.
Huwa ni hedhi ya kwanza na ya mwisho kwa wakati huo, haitatokea tena hadi binti huyo atakapo fikia umri wa kuvunja ungo.
Pamoja na kuonekana kwa hedhi hii ya uongo, baadhi ya watoto huonekana pia wakiwa wamevimba matiti yao, na wengine wakienda mbali zaidi kwa kutoa matone ya majimaji mara kwa mara.
Jambo hili hutokea kwa jinsia zote. Ni hali ya kawaida pia, hupona yenyewe tu baada ya siku au wiki chache.
Nini Kifanyike?
Sehemu za siri za mtoto zinapaswa kufanyiwa usafi wa hali ya juu.
Hakuna haja ya kuingia ndani sana wakati wa kumsafisha maana sehemu hizi tangu utotoni huwa na utaratibu wa kujisafisha zenyewe kwenye sehemu zake za ndani.
Maji yenye joto la wastani yanaweza kutumika bila sabuni.
Wazazi wanashauriwa pia kumsafisha mtoto baada ya kujisaidia kutoka mbele kwenda nyuma ili kuzuia kuingia kwa mabaki ya sehemu ya haja kubwa pamoja na vijidudu vya magonjwa kwenye uke.
Hii itamkinga mtoto dhidi ya maambukizi ya mara kwa mara hasa yale ya mfumo wa mkojo yaani UTI.
Muhtasari
Kama damu au uchafu huo utakuwa na harufu kali sana, mtoto huyo apataswa kufikishwa hospitalini haraka.
Pia, ikiwa damu au uchafu huo utakuwa mwingi sana, utaendelea kutoka kwa zaidi ya siku mbili na kama mtoto atakuwa kapata homa au hali yake ya afya itakuwa imebadilika ni lazima pia awahishwe hospitalini kwa uchunguzi na matibabu.