Pamoja na uwepo wa tofauti nyingi zinazoambatana na takwa hili la asili na kibaiolojia linalotokea kwa wanawake, bado tunaweza kuunganisha kwa pamoja makundi manne ya tabia zinazoongoza kutokea kwake.
Tabia hizo ni kama ifuatavyo;
- Idadi ya siku za kutoka kwa damu
- Muonekano wa damu
- Kiasi cha damu
- Utaratibu wa utokaji wa damu
1. Idadi ya Siku
Idadi ya siku ambazo damu ya hedhi hutoka hutofautiana kati ya mwanamke mmoja na mwingine.
Idadi ya siku za kawaida ni 3-7 hivyo kwa wanawake wanaopata hedhi chini ya siku 3 au zaidi ya siku 7 ni vyema wakienda hospitalini kufanya uchunguzi wa afya zao. (1)
2. Muonekano wa Damu
Damu ya hedhi kwa kawaida huwa na rangi nyekundu ambayo inaweza kuwa imekolea sana, au inaweza kuwa imepauka.
Kwa lugha rahisi kabisa, rangi yake haina tofauti kubwa na rangi ya damu inayovuja baada ya kujikata na kisu, au unapopata ajali.
Inaweza pia kuwa na rangi ya brown (kahawia) kwa baadhi ya wanawake na ikawa sawa.
Damu hii haipaswi kuwa na harufu kali sana ya kutisha.
Inaweza kutoka ikiwa imeganda kidogo, lakini kama damu hii inatoka na mabonge makubwa ya damu msaada wa kitabibu unahitajika kuchunguza hali hii.
3. Kiasi cha Damu
Wastani wa ujazo wa damu unaopotea kila hedhi ni 35 ml. Hata hivyo, kiasi cha kawaida huwa ni kati ya 5-80 ml.
Ikiwa mwanamke anapoteza damu nyingi sana zaidi ya 80 ml hii siyo sawa, atakuwa anakabiliwa na tatizo la kuwa na hedhi nzito ambalo huhitaji uchunguzi wa daktari.
Hali hii inaweza kugunduliwa kwa kufuatilia muda ambao taulo ya kike hutumia ili ilowane damu.
4. Utaratibu wa Damu
Baadhi ya wanawake huwa na siku kadhaa za kutokwa na uchafu mwingine (siyo damu) kabla au baada ya hedhi, hii ni sawa.
Katika mazingira ya kawaida, hedhi huanza kwa damu ndogo ambayo huongezeka kadri muda unavyokwenda.
Damu hii hufikia kipindi cha kubaki na usawa kisha baadae huanza kupungua taratibu kadri siku zake zinavyoelekea mwishoni, hatimaye hukoma kabisa.
Muhtasari
Mambo haya yatumike kama ishara ya kuongoza utaratibu wa kila mwezi wa hedhi ya mwanamke.
Kupata suluhisho la mapema kutazaidia kuweka sawa mzunguko wa hedhi husika.
Hakuna haja ya kujificha, tafuta suluhu ya changamoto yako.