Wastani wa ujazo wa damu unaopotea kila hedhi ni 35 ml.
Hata hivyo, kiasi cha kawaida huwa ni kati ya 5-80 ml. (1)
Ikiwa mwanamke anapoteza damu nyingi sana zaidi ya 80 ml hii siyo sawa, atakuwa anakabiliwa na tatizo la kuwa na hedhi nzito ambalo huhitaji uchunguzi wa daktari.
Sababu
Hali hii inaweza kusababishwa na mvurugiko mkubwa wa homoni mwilini, hasa wakati wa utolewaji wa yai kwa mwezi husika. Mvurugiko huu wa homoni unaweza kupelekea kutengenezwa kwa ukuta mkubwa kwenye mji wa uzazi kuzidi kiasi cha kawaida, hivyo kuongeza kiwango cha damu kinachotolewa wakati wa hedhi.
Pia, matatizo kwenye tezi za thyroi, uwepo wa uvimbe kwenye mji wa uzazi, matumizi ya aina fulani za dawa, mfano dawa za uzazi wa mpango, matatizo ya ujauzito mfano, kuharibika kwa ujauzito, mimba nje ya mji wa uzazi), matatizo katika kuganda kwa damu mfano, haemophilia, kiribatumbo pamoja na matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango mfano vijiti, majira, kitanzi na sindano za depo provera inaweza kuchangia kutokea kwake.
Athari
Upotevu wa damu huenda sambamba na upotevu wa madini chuma.
Hii ndio sababu inayomfanya mwanamke ashauriwe kutumia vyakula na virutubisho vyenye madini mengi ya chuma kila siku kuzidi mwanaume.
Upotevu wa damu nyingi pamoja na upungufu wa madini ya chuma mwilini husababisha dalili zifuatazo kwa mwanamke ambazo mara nyingi hutokea siku chache baada ya hedhi;
Uchovu bila sababu, kupauka kwa rangi ya ngozi, maumivu ya kifua na kichwa, kuongezeka kwa mapigo ya moyo, kuishiwa kwa pumzi, kizunguzungu, pungufu wa damu, kichefuchefu pamoja na kuwa na kucha kavu za mikono na miguu.
Pia, dalili kama kuvimba kwa ulimi, kutikisika kwa miguu na kuwa na mikono na miguu ya baridi sana zinaweza kuonekana.
Muhtasari
Vyanzo vikubwa vya madini chuma ni maini ya wanyama, nyama, vyakula jamii ya karanga, mboga za majani hasa broccoli na spinach, mayai ya kuku pamoja na mbegu za maboga. (3,4)
Ni vyema wanawake wakitumia vyakula hivi kwa wingi ili kuepuka changamoto hizi.