Namna ya Kuhesabu Siku za Hedhi

3 Min Read

Hedhi ni utaratibu wa utokaji wa damu pamoja na uchafu mwingine kwenye sehemu za siri za mwanamke kila mwezi, ambao kwa lugha zingine zilizozoeleka sana huitwa period.

Wakati wa mzunguko wa mwezi wa hedhi husika, kuta za mji wa uzazi hupanuka na kuimarishwa ili ujauzito uweze kutungwa.

Ikitokea ujauzito haujatungwa, kiwango cha vichocheo vya estrogen na progesterone vinavyoongoza na kulinda mzunguko wa hedhi hii hupungua sana kwenye damu.

Kupungua kwa vichocheo hivi huuambia na kuuamuru mwili wa mwanamke utoe hedhi kwa kuubomoa mji wa uzazi ulioshindwa kutimiza tarajio la kazi yake mwezi ule ya kuhifadhi ujauzito.

Utaratibu huu huendelea kila mwezi isipokuwa wakati wa ujauzito, muda fulani baada ya kujifungua na pindi mwanamke afikiapo umri wa ukomo wa hedhi.

Hedhi ya kwanza ya msichana huanza mara baada ya kuvunja ungo, kati ya umri wa miaka 8 hadi 15, hii ni wastani wa miaka miwili baada ya kuchomoza kwa matiti na kuota kwa nywele za sehemu za siri.

Idadi ya Siku

Kuna aina nyingi ya mizunguko ya hedhi ambayo huchukua wastani wa siku 21-35. Hii haitoi maana ya moja kwa moja kuwa wasiopata ndani ya muda huu wanakuwa na matatizo ya kiafya, kwani baadhi ya wanawake hutumia hadi siku 45 kupata hedhi zao.

Pamoja na utofauti huu mkubwa, bado namba zinautaja mzunguko wa siku 28 kuwa ndiyo mzunguko unaopatikana walau kwa kundi kubwa la wanawake kuliko mizunguko mingine.

Unahesabu Vipi?

Hedhi huanza kuhesabiwa toka siku ya kwanza ya kutokwa na damu kwa mwezi fulani hadi siku moja kabla haijaaza tena kutoka kwa mwezi mwingine.

Mfano, kama leo ndio damu imetoka kwa mara ya kwanza, chukua siku hii kama siku ya kwanza, kesho ikiendelea chukua siku hiyo kama siku ya pili, kesho kutwa kama damu inaendelea kutoka chukua siku hiyo kama siku ya tatu.

Endelea kuhesabu idadi ya siku hizi hadi siku moja kabla haijaanza tena kutoka kwa mwezi mwingine bila kujali damu imeacha lini kutoka.

Hii inamaanisha kuwa, hata kama damu ya hedhi huchukua siku 5 kukoma, unapaswa kuendelea kuhesabu siku bila kuacha hadi siku moja kabla haijaanza tena kutoka kwa mwezi mwingie.

Muhtasari

Kwa wanawake ambao siku zao hutofautiana kila mwezi, mfano mwezi mmoja anapata siku 26, mwezi mwingine siku 28 na mwezi mwingine siku 30 wanapaswa kuzijumlisha kwa pamoja kupata wastani.

Mfano (26+28+30) utapata 84.

Namba hii ukiigawa kwa 3 utapata 28 hivyo wastani wa siku za mzunguko itakuwa ni siku 28. Kumbuka, utaratibu wa kuhesabu siku za hedhi ni uleule kama tulivyoona hapo juu.

Share This Article