Mambo 11 ya Kuzingatia kwa Mjamzito ili Ajifungue Salama

5 Min Read

Kuna mambo mengi ambayo hutokea wakati wa ujauzito, pia huwepo stori nyingi sana ambazo wanawake wajawazito husikia, huambiwa au hata kuzisoma sehemu mbalimbali.

Achana na habari hizo, zingatia mambo haya 10 ili yawe nguzo muhimu katika kufanikisha uzazi salama.

1. Mazoezi

Jitahidi kufanya mazoezi kila siku wakati wote wa ujauzito.

Vitu kama kutembea, kuogelea na mambo mengine madogo madogo kama haya huimarisha misuli hivyo kukufanya uwe tayari kuhimili changamoto zote za kujifungua. (1,2)

Ikiwa umeshauriwa hospitalini kuwa ni lazima upate muda wa kupumzika, hakikisha unafuata ushauri huu.

2. Hewa

Fanya mazoezi ya kuvuta hewa ya kutosha hasa kwa kutumia kifua na tumbo, jaribu kufanya mazoezi ya kuvuta na kutoa hewa kwa nguvu kila siku. (3)

Utakuwa umejiandalia mazingira mazuri ya kukabiliana na suala la kupungukiwa na hewa wakati wa kusukuma mtoto.

3. Chakula

Kula chakura bora kila siku hasa matunda, mboga za majani, vyakula vyenye utajiri wa madini chuma na protini. (4,5,6)

Ni muhimu kwa afya ya mama pamoja na mtoto aliyeko tumboni.

Epuka kula vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi.

4. Uzito

Jitahidi uwezavyo kuutunza uzito wako. Zuia kwa nguvu zote kuongezeka uzito uliopitiliza.

Hii itakufanya ujitengenezee mazingira ya kujifungua kwa upasuaji. Mara nyingi uzito huongezeka wakati wa ujauzito, hii ni kawaida. (7,8)

Uzito tunaosema hapa ni ule usiosababishwa na ujauzito.

5. Hadithi

Jiepushe na stori au hadithi hasa zile zinazosimuliwa na rafiki zako (waliowahi kuzaa) kama vile maumivu makali ya uchungu wa kujifungua, utokwaji wa damu, kuzaa kwa upasuaji na mambo mengine kama haya yanayoweza kukufanya uanze kujutia uamzi wako wa kushika ujauzito.

Unachopaswa kufanya ni kuishi kwa amani na furaha kwani kila mtu hupatwa na jambo hili kwa namna yake. (9,10)

Kumbuka, stori wanazopeana wanawake (wenyewe) clinic na mitaani nyingi sana huwa za uongo au kutishana.

6. Taarifa

Anza kujifunza na kufuatilia taarifa zote hasa zinazohusu namna gani ya kukabiliana na uchungu, hatua zake pamoja na mambo yote ambayo hutokea wakati huu.

Itakufanya usiwe mgeni na kukupunguzia paniki, pia itasaidia kuwa na ujuzi wa awali utakao saidia kwenye kumlea na kumtunza mtoto. (11)

7. Msaada

Anza kutafuta watu watakaokuwa karibu na wewe muda wote wakikuongoza na kukutia moyo, acha kujitenga na jamii yako kwani siku ya uchungu huwa haijulikani.

Inaweza kukukuta bila maandalizi yoyote na ikawa changamoto kubwa kwako.

Ni lazima ujue pia hospitali, mtu atakayekuongezea damu ikiwa atahitajika pamoja na kuandaa usafiri wa kukufikisha huko kituoni. (12)

8. Mapumziko na Magonjwa

Jitahidi upate muda mwingi wa kupumzika, tunza usafi wa mwili wako kila siku.

Pia jikinge na magonjwa hasa yale yanayosababishwa na ngono kama vile kaswende, kisonono na pangusa ambayo ni hatari sana wakati wa kujifungua. (13,14)

Upumzike kwa masaa mangapi? Yoyote yale ambayo utaona yanafaa kwako.

9. Maji

Yafanye maji kuwa rafiki yako mkubwa.

Kunywa maji ya kutosha kutakufanya usipungukiwe na maji wakati wa kujifungua pia uwe na nguvu za kutosha, huku kuoga mara kwa mara kutakufanya utunze joto lako la mwili kikamilifu. (15)

Unapokuwa na maji ya kutosha unakuwa pia unaongeza ujazo wa damu yako.

Kumbuka kuwa damu nyingi sana hupotea wakati wa kujifungua.

10. Wasiwasi

Wasiwasi unaweza kukufanya upitie wakati mgumu kipindi chote cha ujauzito pamoja na kujifungua.

Ondoa wasiwasi, utajifungua salama. (16)

11. Fika Kliniki

Hudhuria kilini za uzazi mara kwa mara uweze kupata ujuzi wa mambo mbalimbali pamoja na kufuatilia kwa ukaribu uthabiti wa afya yako.

Husaidia kugundua mapema changamoto za ujauzito pamoja na kutafuta majibu ya haraka katika kuhakikisha kuwa afya ya mama na mtoto zipo salama.

Hudhurio la walau kliniki 3 za ujauzito hufaa kwenye kipindu chote cha ujauzito.

Muhtasari

Kuuleta uhai mpya duniani ni hadhi ya kipekee aliyopewa mwanamke.

Kwa maana hiyo, zoezi lako la kujifungua litafanikiwa kwa ufanisi mkubwa pasipo shida yoyote.

Baada ya safari yako ya kuubeba ujauzito huu kwa zaidi ya siku 280, sasa upo tayari kuwa mama.

Share This Article