Asilimia 60 ya mwili wa binadamu ni maji. Unywaji wa maji ya kutosha kila siku ni muhimu kwa afya ya binadamu yeyote yule.
Ukiondoa faida zingine za maji kwenye mwili wa binadamu, maji huhusika kwa kiasi kikubwa sana katika kuboresha na kuamua uhai wa afya ya uzazi.
1. Wanaume
Upungufu wa maji mwilini husababisha uzalishwaji hafifu wa shahawa.
Kama mbegu za kiume zitabebwa na shahawa nzito sana, uwezo wake wa kuogelea hupungua hivyo kuhatarisha uimara wa afya ya uzazi hasa uwezo wa kurutubisha yai.
2. Mtoto tumboni
Maji huhitajika tokea siku ya kwanza ya kutungwa kwa ujauzito. Husaidia usafirishwaji na ubadilishanaji wa virutubisho, uchafu na hewa kati ya mama na mtoto.
Uchache wa maji huhatarisha ujauzito na kuongeza uwezekano wa kuharibika kwake (miscarriage).
3. Wanawake
Maji huwa ni sehemu muhimu sana ya kuboresha, kutunza na kuimarisha afya ya mwili na uzazi kwa ujumla.
Uchache wa maji mwilini huathiri utolewaji wa mayai kila mwezi ama kwa kuchelewa, kuwahi au kutokutolewa kabisa.
Maji husaidia pia utengenezwaji wa ute wezeshi kwa mbegu za kiume ziweze kuogelea vizuri pale zinapotolewa wakati wa siku zenye uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ujauzito.
Ute huu pia hurekebisha uwiano wa pH kwenye uke ili usiwe na asidi nyingi sana kuzuia mbegu za kiume zisiuliwe Ili kijusi kiweze kuhifadhiwa vizuri kwenye mji wa uzazi, ni lazima seli za kuta za mji wa uzazi zijigawe na kubadili tabia zake, pia ni lazima ziwe imara na afya bora kabisa.
Maji ni muhimu sana katika kuwezesha utimilifu wa mambo haya yote.
Kiasi cha Maji
Taarifa za kiasi sahihi cha kiasi cha maji unachopaswa kunywa kila siku huelezewa tofauti tofauti na vyanzo mbalimbali kulingana na uzito au umri wa mhusika.
Lakini kuondoa sintofahamu hii, kiasi cha lita 2.5 kwa siku hufaa sana kwa afya ya binadamu bila kujali jinsia yake.