Mwili wa binadamu huhitaji madini ya sodium yanayopatikana kwenye chumvi ili kuwa na afya bora.
Pamoja na umuhimu huu, matumizi ya chumvi nyingi yanaweza kusababisha kutokea kwa shinikizo kubwa la damu.
Unapotumia chumvi nyingi maana yake unaupa mwili wako madini mengi ya sodium zaidi ya inavyotakiwa. (1,2,3)
American Heart Assosiation wanashauri matumizi ya chumvi yasizidi kiasi cha wastani wa 1.5 gramu kila siku. (4)
Madhara
Chumvi ikizidi sana huupa mwili kazi ya ziada ya kutunza maji mengi ili kuipunguzia nguvu. Jambo hili huongeza msukumo wa damu hivyo kusababisha mtu augue shinikizo kubwa la damu.
Unapokuwa na hali hii, magonjwa mengine nyemelezi yanakuwa na nafasi kubwa sana ya kukusumbua ambayo ni magonjwa ya moyo, kiharusi, kuacha kufanya kazi kwa moyo pamoja na kudhoofika kwa afya ya mifupa hivyo kuongeza hatari ya kuvunjika kutokana na kutolewa kwa madini ya calcium ili kufidia kiasi cha sodium kilichozidi.
Aidha, matatizo ya figo, saratani, kuongezeka kwa uzito na kupungua kwa uwezo wa ubongo hasa katika kutunza kumbukumbu hutokea. (5,6)
Tumia chumvi ya kawaida tu kila siku, hakuna haja ya kutumia nyingi sana. Hii ni wastani wa kijiko kimoja tu.
Hii ni muhimu katika kuukinga mwili wako dhidi ya magonjwa mengi, hasa yale yasiyoambukiza.