Ugonjwa wa Trichomoniasis

3 Min Read

Ni miongoni mwa magonjwa maarufu zaidi ya zinaa yasiyo sababishwa na virusi.

Ni chanzo muhimu cha uambukizwaji wa VVU na changamoto za uzazi hasa kwa wanawake.

Chanzo

Husababishwa na kimelea chenye seli moja ya protozoa kiitwacho Trichomonas vaginalis. (1,2)

Uke ni sehemu yenye hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa, kwa wanaume sehemu hatari zaidi ni njia ya mkojo.

Kwa miaka mingi imekuwa inaaminika kuwa kimelea hicho husambazwa kupitia ngono pekee, lakini tafiti za sasa zinathibitisha kuwa kutumia maji yaleyale ya kuoga ambayo mgonjwa ameyatumia pamoja na kuchangia vifaa vya kuogea hasa sabuni huchangia kusambaa wa vimelea hivi. (3,4,5)

Takwimu

Wastani wa watu milioni 276 huambukizwa ugonjwa huu kila mwaka. (6

Dalili

Ugonjwa huu huwa na dalili nyingi, zinazotofautiana kulingana na ukubwa wa tatizo kwa wakati huo. Baadhi ya watu huwa hawaoneshi kabisa dalili zozote lakini wengine huzionesha kati ya siku ya 5-28 tangu kupatwa na maambukizi.

Ukosefu huu wa dalili huongeza hatari ya kukua kwa ugonjwa, pamoja na kuongezeka kwa mnyororo wa maambukizi.

Miongoni mwa dalili hizo ni uke kutoa uchafu usio wa kawaida ambao mara nyingi huwa na rangi ya njano, uume kutoa uchafu mweupe, kuwasha kwa mashavu, midomo ya uke na uume pamoja na kupata harufu kali ukeni inayofanana na kisamaki.

Pia, uwepo wa maumivu makali wakati wa kukojoa, kuvimba kwa mashavu na midomo ya uke pamoja na kubadilika kwa rangi ya kuta za mlango wa kizazi kuwa na rangi nyekundu sana ni miongoni mwa dalili za uwepo wa ugonjwa huu.

Tiba

Unaweza kutibiwa kwa kutumia madawa ya kuua vimelea hivyo.

Baadhi ya dawa zinazoweza kutumika ni metronidazole, tinidazole pamoja na dawa zingine za antibayotiki.

Mhudumu wa afya atakuelekeza matumizi sahihi ya dawa pamoja na dozi sahihi kwa kadri atakavyoona inafaa.

Kinga

Unataka kujikinga na ugonjwa huu? Fanya mambo yafuatayo;

  • Kuwa mwaminifu, tulia na mpenzi mmoja.
  • Wakati wa matibabu, ni vizuri ukijizuia wewe na mwenzi wako kushiriki tendo la ndoa ili
    kuepuka nafasi ya kuambukizana tena. Inafaa msubiri hadi ugonjwa upone.
  • Tumia kinga.

Muhtasari

Unaweza kuugua ugonjwa huu zaidi ya mara moja hata baada ya kupata tiba. Ili kuzuia maambukizi ya kujirudia, ni lazima wapenzi wote watibiwe kwa pamoja.

Ugonjwa huu usipotibiwa huongeza nafasi ya kushambuliwa na VVU.

Kwa wanawake wajawazito huongeza nafasi ya kujifungua kabla ya wakati pamoja na kujifungua watoto wenye uzito mdogo.

Pata tiba sahihi.

Share This Article