Neno sahihi kwa kiingereza ni Genital Warts.
Ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na virusi vinavyofahamika kama Human papillomavirus (HPV) ambavyo kwa ujumla wake, hupatikana katika aina tofauti zaidi ya 100. (1)
Hivi ni vinyama vidogo vinavyoota kwenye ngozi au utando laini unaozunguka maeneo ya sehemu za siri.
Uambukizwaji
Ugonjwa huu unaweza kudhuru uume, uke, mlango wa uzazi, sehemu ya haja kubwa, mrija wa mkojo, midomo, koo, pamoja na kibofu cha mkojo.
Husambazwa kwa mgusano wa ngozi kwa ngozi hasa wakati wa ngono, japo migusano mingine ya maeneo athirika isiyohusisha ngono inaweza pia kuwa chanzo cha kusambaa kwake.
Virusi wanaosababisha ugonjwa huu huwa na uhusiano wa moja kwa moja na kutokea kwa saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya koo, uke, uume pamoja na saratani ya njia ya haja kubwa, hivyo ni vyema wagonjwa wakatibiwa haraka na kwa usahihi ili kuepusha changamoto hizi. (2,3)
Hivyo, kuwa makini unaposhiriki tendo la ndoa na mtu usiye na uhakika wa afya yake.
Dalili
Dalili kubwa ni kuota kwa nyama kwenye sehemu za siri ambazo zinaweza kuwa ndani ya uke, nje ya uke, mlango wa kizazi, sehemu ya haja kubwa pamoja na sehemu inayopatikana kati ya uke na sehemu ya haja kubwa.
Dalili zingine ni;
- Miwasho sehemu husika
- Kuchomwachomwa sehemu husika
- Kutokuhisi maumivu (kufa ganzi) maeneo yanayozunguka masundosundo
- Kuvuja damu ukeni baada ya tendo la ndoa
Tiba
Unaweza kutibiwa kwa kutumia madawa mfano Podophyllotoxin, Podophyllin, 5-fluorouracil na Thiotepa.
Mhudumu wa afya ataelezea matumizi sahihi ya dawa pamoja na dozi sahihi kwa kadri atakavyoona inafaa.
Masundosundo yanaweza pia kutibiwa kwa upasuaji mdogo, kukausha kwa njia ya barafu, umeme au kwa mionzi maalumu.
Kinga
Kuwa mwaminifu, tulia na mpenzi mmoja na tumia kinga mara kwa mara.
Wakati wa matibabu, ni vizuri ukijizuia wewe na mwenzi wako kushiriki tendo la ndoa ili kuepuka nafasi ya kuambukizana tena. Inafaa
msubiri hadi ugonjwa upone.
Watu wote walioshiriki tendo la ndoa na mhusika wanapaswa kuchunguzwa na kupata tiba kwa pamoja, ikiwa itaonekana kuna uhitaji huo baada ya kuchunguzwa.
Aidha, ipo chanjo maalumu inayoweza kukinga ugonjwa huu. Kwa vijana wa miaka 9-26 wanaweza kuipata. (4)
Muhtasari
Unaweza kuugua ugonjwa huu zaidi ya mara moja hata baada ya kutumia vizuri dawa na kupona.
Masundosundo yaliyo ndani ya mlango wa kizazi hubadilisha kabisa eneo hilo na huongeza uwezekano wa kuugua saratani ya mlango wa kizazi.
Ikiwa mwanamke mjamzito atakuwa na ugonjwa huu kisha akashindwa kuutibu vizuri, mfereji wa uzazi unaweza kuzibwa na nyama hizi.
Hii inaweza kumfanya ajifungue kwa upasuaji au kuathirika kwa mfumo wa upumuaji wa mtoto. (5,6)
Pata tiba sahihi.