Ugonjwa wa Klamidia (Chlamydia)

3 Min Read

Neno sahihi kwa kiingereza ni Chlamydia.

Ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na viini vya bakteria vijulikanavyo kama Chlamydia trachomatis. (1)

Uambukizwaji

Husambazwa kwa njia ya ngono ya uke, mdomo pamoja na sehemu ya haja kubwa. Pia, mama mjamzito anaweza kumuambukiza mtoto wakati wa kujifungua hivyo kusababisha nimonia kali, pia maambukizi kwenye macho ya mtoto mchanga.

Majimaji ya sehemu za siri za mgonjwa yanaweza pia kuambukiza sehemu zingine za mwili, mfano macho kwa kujigusa.

Usipotibiwa unaweza kusababisha utasa au ugumba kwa jinsia zote.

Dalili

Asilimia 40-96 ya wagonjwa huwa hawaoneshi dalili zozote. (2)

Kwa kawaida hatua za awali za ugonjwa huu hazina dalili, huanza kuonekana walau siku 5-10 baadae.

Miongoni mwa dalili za uwepo wa ugonjwa huu ni uwepo wa maumivu makali ya tumbo, kuvuja damu kabla ya siku za hedhi kuhisi uchungu wakati wa tendo la ndoa pamoja na uchungu au kujihisi kuchomwa wakati wa haja ndogo.

Aidha, dalili zingine ni kujisikia kwenda haja ndogo kila mara, kuvuja damu ukeni baada ya tendo la ndoa, kutokwa na usaha wa manjano kwenye mlango wa uzazi ambao unaweza kuwa na harufu kali pamoja na vimbe, pia kuvuja damu sehemu ya haja kubwa.

Tiba

Unaweza kutibiwa kwa kutumia madawa ya antibayotiki hasa Azithromycin na Doxycyline.

Mhudumu wa afya ataelezea matumizi sahihi ya dawa pamoja na dozi sahihi kwa kadri atakavyoona inafaa.

Kinga

Unaweza kujikinga na ugonjwa huu kwa kuwa mwaminifu, tulia na mpenzi mmoja pamoja na kutumia kinga mara kwa mara.

Pia, wakati wa matibabu, ni vizuri ukijizuia wewe na mwenzi wako kushiriki tendo la ndoa ili kuepuka nafasi ya kuambukizana tena. Inafaa msubiri hadi ugonjwa upone.

Wanawake wanashauriwa kuaacha kudeki uke (Kujisafisha kwa kutumia pombe, apple cider vinegar, magadi soda, iodine pamoja na kemikali zingine)

Kwa baadhi ya wanawake, maambukizi ya ugonjwa huu husambaa hadi kwenye mirija ya uzazi na kusababisha ugonjwa wa PID.

Ugonjwa huu ni chanzo cha ugumba na kuharibika kwa ujauzito kwa wanawake wengi.

Ni muhimu kuutibu vizuri ili kuepusha madhara ya muda mrefu yanayoweza kuathiri sehemu nyingi za mwili ikiwemo mfumo wa uzazi.

Muhtasari

Kila mtu anayeshiriki tendo la ndoa anaweza kuugua ugonjwa huu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya maambukizi milioni 1 ya magonjwa ya zinaa hutokea kila siku.

Ugonjwa wa klamidia upo pia kwenye orodha hiyo hivyo ni muhimu kujilinda ipasavyo.

Share This Article