Ugonjwa wa Kisonono (Gonorrhea)

4 Min Read

Neno sahihi kwa kiingereza ni Gonorrhea.

Ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na viini vya bakteria vijulikanavyo kama Neisseria gonorrheae.

Husambazwa kwa njia ya mgusano wa via vya uzazi yaani tendo la ndoa kupitia uke, mdomo pia sehemu ya haja kubwa.

Watoto wanaweza kupata ugonjwa huu kutoka kwa mama zao wakati wa kujifungua. (1,2)

Athari

Ugonjwa huu unaweza kudhuru uume, uke, mlango wa uzazi, sehemu ya haja kubwa, mrija wa mkojo, jicho au koo.

Usipotibiwa unaweza kusababisha utasa, kushambuliwa na magonjwa ya mfumo wa uzazi hasa PID, ugumba au kutokuwa na uwezo wa kurutubisha kwa wanawake na wanaume. (3,4)

Dalili

Huwa hazionekani upesi, zinaweza kutokea kati ya siku 2- 14 tangu kuambukizwa kwa mara ya kwanza.

Miongoni mwa dalili zake ni uwepo wa maumivu ya tumbo, kuvuja damu kabla ya hedhi, matatizo ya hedhi, kuhisi uchungu au maumivu makali wakati wa tendo la ndoa na wakati wa haja ndogo, kutapika pamoja na kutokwa na usaha ukeni ulio na rangi ya manjano au manjano hafifu.

Aidha, dalili zingine ni kuwashwa na kuvimba kwa mashavu au midomo ya uke, kuvimba na kuwashwa sehemu ya haja kubwa, usaha na uchungu wakati wa haja kubwa.

Baadhi ya watu huwashwa kwa koo, vidonda kooni na shida ya kumeza zinaweza kuwa dalili za uwepo wa maambukizi haya kwenye sehemu ya koo.

Tiba

Unaweza kutibiwa kwa kutumia madawa (viua vijasumu- antibiotics) mfano Azithromycin, ceftriaxone na gentamicin.

Mhudumu wa afya ataelezea matumizi sahihi ya dawa pamoja na dozi sahihi kwa kadri atakavyoona inafaa.

Kinga

Unaweza kujikinga dhidi ya ugonjwa huu kwa kuwa mwaminifu, kutulia na mpenzi mmoja pamoja na kutumia kinga.

Wakati wa matibabu, ni vizuri ukijizuia wewe na mwenzi wako kushiriki tendo la ndoa ili kuepuka nafasi ya kuambukizana tena. Inafaa msubiri hadi ugonjwa upone.

Aidha, watu wote walioshiriki tendo la ndoa na mgonjwa ndani ya siku 60 wanapaswa kujulishwa ili wapimwe, ikibainika kuwa na ugonjwa na huu matibabu yataanza mara moja. Watu wote walioshiriki tendo la ndoa na mhusika ndani ya wiki 2 za nyuma wanapaswa kujulishwa ili wao pia waanze tiba mara moja.

Wanawake

Kila mwanamke anayeugua kisonono huwa na hatari ya kupatwa na madhara ya muda mrefu ya ugonjwa huu.

Hushambulia via vya uzazi na mfumo mzima wa uzazi ukihusisha uke, mji wa uzazi, mirija ya mayai pamoja na vifuko vya mayai.

Madhara haya yanaweza kusababisha kutokea kwa ugonjwa wa PID ambao hudumaza uhai wa afya ya uzazi pamoja na kusababisha maumivu ya kudumu ya tumbo.

Huziba mirija ya mayai, husababisha ugumba au kuhifadhiwa kwa ujauzito nje ya mji wa uzazi.

Ni muhimu sana kama tiba sahihi itatolewa, kwa wakati sahihi.

Muhtasari

Ugonjwa wa kisonono unaweza kusambaa hadi kwenye macho.

Hutokea hasa baada ya kusugua sehemu za siri kisha ukagusa macho kabla ya kujisafisha mikono.

Dalili za kisonono cha macho ni miwasho, kuvimba kwa kope na macho, wekundu wa macho pamoja na kutoka kwa uchafu au usaha mweupe au manjano kwenye macho.

Aina zote za ugonjwa huu zinatibika.

Share This Article