Kwa Kiswahili hufahamika zaidi kama maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo wa uzazi wa mwanamke ikihusisha mlango wa kizazi, mji wa uzazi, mirija ya uzazi pamoja na vifuko vya mayai ya uzazi.
PID hutokea baada ya kupanda juu kwa bakteria wabaya kutoka kwenye uke na mlango wa kizazi kwenda kwenye kuta za mji wa uzazi na mirija ya uzazi.
Uambukizwaji
Neisseria gonorrhoeae, Chlamydia trachomatis na Mycoplasma genitalium ndiyo vijidudu hatari zaidi kwa kusababisha PID, na husambazwa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kwa njia ya ngono, hivyo uwepo wa magonjwa ya zinaa hasa Kisonono na Klamidia huchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa ugonjwa wa PID.
Mtu anaweza pia kupata ugonjwa huu kutokana na uwepo wa maambukizi makali baada ya kutoa ujauzito, kuharibika kwa ujauzito au baada ya kufanyika kwa utaratibu wowote ule unaofungua tumbo. (1,2,3)
Katika hali chache, bakteria wazuri wanaopatikana kwenye uke wanaweza kugeuka wabaya ikiwa watavuka mlango kwa kizazi na kuingia sehemu ya juu ya viungo vingine.
PID inaweza kusababisha ugumba, utasa, maumivu ya kudumu ya tumbo la chini na nyonga pamoja na kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi.
Ni vizuri ikishughulikiwa vizuri, mapema na kwa usahihi. (4,5)
Dalili
Dalili za ugonjwa huu hutofautiana kulingana na hatua husika. Sio kila mwanamke huonesha dalili za kufanana na mwingine.
Pamoja na uwepo wa tofauti hizi, dalili za ujumla za ugonjwa huu ni uwepo wa maumivu makali sehemu ya chini ya tumbo, homa kali kutokwa na damu katikati ya mzunguko wa hedhi, mlango wa kizazi huwa mwekundu sana, ambao mara nyingi hutoa uchafu mzito wenye rangi ya njano-kijani, kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi, baadhi ya wanawake huwa hawaoneshi dalili kubwa, na hudhani kuwa wapo sawa kabisa. Changamoto huja wakati wa kutafuta ujauzito, wengi hushitushwa na ugumu katika kufanikisha zoezi hili pamoja na aumivu wakati wa haja ndogo na wakati wa tendo la ndoa.
Tiba
PID inaweza kutibiwa kwa kutumia madawa (viua vijasumu-antibiotics) mfano Azithromycin, Ceftriaxone, Clindamycin, Gentamicin na Doxycyline.
Mhudumu wa afya atakuelekeza matumizi sahihi ya dawa pamoja na dozi sahihi kwa kadri atakavyoona inafaa.
Kinga
Njia za kujikinga na ugonjwa huu zipo wazi. Unaweza kujikinga kwa kuwa mwaminifu, tulia na mpenzi mmoja.
Pia, wakati wa matibabu, ni vizuri ukijizuia wewe na mwenzi wako kushiriki tendo la ndoa ili kuepuka nafasi ya kuambukizana tena. Inafaa msubiri hadi ugonjwa upone.
Ili kukata mnyororo wa maambukizi, ni vizuri wapenzi wote wakitibiwa kwa pamoja. Ni muhimu kukumbuka kuwa,wanaume hawawezi kuugua PID lakini huwa na uwezo wa kubeba bakteria wanaosababisha tatizo hili na kuwapitisha kwa mwanamke wakati wa tendo la ndoa.
Muhtasari
Ni muhimu pia mwanamme akienda hospitalini kuchunguzwa pamoja na mwanamke kwani anaweza kuwa chanzo cha ugonjwa huu. (6)
Aidha, siyo kila uchafu mweupe, manjano au kijani unaotoka ukeni humaanisha PID, pia siyo kila maumivu yanayotokea chini ya tumbo, kutokwa na damu au hata uwepo wa maumivu makali wakati wa tendo la ndoa huwa wa PID.
Epuka kununua vitu dukani, mitandaoni au mtaani bila kupima kwanza hospitalini, utaumia.